Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt Rehema Nchimbi amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kuanzisha operesheni maalumu ya kuwapima macho wakazi wote Mkoani hapa hususani watumishi wa serikali.
Dkt Nchimbi ametoa agizo hilo mapema jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani ambapo asilimia 94 ya watu wenye upofu Mkoani Singida wanasumbuliwa na matatizo ya macho ambayo yanazuilika.
Amesema ili watumishi wa umma waweze kutoa huduma iliyo bora wanatakiwa kuwa na uoni mzuri hivyo kuwapima ni hatua kubwa itakayosaidia kutibu na kuzuia upofu mapema.
“Mganga Mkuu wa Mkoa sasa tunataka uanzishe operesheni tupimwe wote macho, inasikitisha kusikia hao wote waliopata upofu takribani watu elfu 25 wangeweza kupona endapo wangegundulika mapema kwakuwa matatizo yaliyowasababishia upofu yanazuilika”, amesema Dkt Nchimbi na kusisitiza kuwa,“Halmashauri zote tengeni bajeti za kununua dawa za macho pamoja na kuhakikisha wananchi wenu wote wanapimwa macho ili magonjwa yanayozuilika yapewe matibabu mapema, watendaji msione fahari kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa macho wakati mngeweza kuwasiadia”, ameeleza Dkt Nchimbi.
Awali, Dkt Nchimbi amepokea kifaa cha kisasa aina ya Auto Perimeter Glautefield Lite kutoka kwa Shirika la Sight Saver, chenye uwezo wa kuona taswira na matatizo ya macho vizuri, ambacho kwa nchi nzima kinapatikana mkoani Singida peke yake.Amesema kifaa hicho kitawasaidi madaktari bingwa wa macho Mkoani hapa kutoa huduma bora huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapatiwe huduma kwani uwepo wa kifaa hicho bila kutumika kitakuwa hakina manufaa.
Dkt Nchimbi ameongeza kuwa, kutokunywa maji ya kutosha husababisha uoni hafifu ambao hupelekea upofu unaozuilika, hivyo amelishauri shirika la Sight Savers kuweka mpango wa kuboresha upatikanaji wa maji na kufanya utafiti hasa maofisini endapo watumishi wanakunywa maji ya kutosha kwakuwa yanasaidia kuzuia upofu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akipokea kifaa cha kisasa cha vipimo vya macho aina ya Auto Perimeter Glautefield Lite kutoka kwa Shirika la Sight Saver, aliyeshika kipaza sauti ni Meneja Mipango na Uendeshaji wa Shirika la Sight Savers Nchini Mhandisi Koronel Kema.
Daktari wa macho akimfanyia uchunguzi wa macho mmoja kati ya wagonjwa waliojitokeza katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Mkoani Singida.
Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho Said Mwiru akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Singida (hayupo pichani) kuwa anaweza kuona na kuwatambua watu kwa kutumia jicho alilofanyiwa upasuaji. Kabla ya upasuaji huo Mwiru amesema jicho hilo lililkuwa halioni.
Baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa macho wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida (hayupo pichani) katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani, akina mama hao wamefanyiwa upasuaji kwa hisani ya shirika la Sight savers.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...