Serikali imesema itahakikisha inaendelea kuwasimamia wakandarasi wa Ujenzi wa
Barabara kuhakikisha wanajenga barabara zote nchini kwa viwango vilivyokusudiwa
na kumaliza kwa wakati ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa leo jijini Dar es salaam baada ya kukagua Awamu ya Tatu ya utekelezaji
wa Ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano jijini humo ambapo ameridhishwa
na kasi ya utekelezaji wake na kusisitiza kwa Wakala wa Baraba (TANROADS), mkoa
wa Dar es salaam kuwa wakali katika usimamizi ili kuhakikisha barabara hizo
zinajengwa kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mkataba.
“ Serikali imekuwa ikitumia Fedha nyingi katika kutekeleza miradi hii, hivyo
TANROADS hakikisheni mnasimamia wakandarasi hawa kujenga barabara hizi kwa
viwango na kwa wakati”, amesema Waziri Mbarawa.
Aidha, Waziri Mbarawa amefafanua kuwa utekelezaji wa awamu hiyo unaendelea vizuri
ambapo unahusisha barabara ya Kifuru – Msigani (km 4.5) ambayo kwa sasa imefika
asilimia 87, Goba – Makongo (km 4.5), nayo imefikia asilimia 52 na Goba – Madale (km
5) yenye asilimia 5.
Profesa Mbarawa ametoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa
Mkandarasi naTANROADS mkoa wa Dar es salaam wakati mradi huo ukiendeleaa
kutekelezwa ili kusaidia kumaliza kwa wakati.
Waziri Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kushughulikia suala la ulipaji wa
fidia kwa wananchi wa maeneo hayo ambao wamepitiwa na mradi huo.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi Julius
Ndyamkama, amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa watasimamia mradi huo usiku na
mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyo bora.
Mhandisi Ndyamkama amebainisha changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa
mradi huo ikiwemo suala la ulipaji wa fidia kwa baadhi ya maeneo hasa katika kipande
cha barabara chenye urefu wa kilometa 1 kuanzia Mto Mbezi kuelekea Makongo.
Naye, Mratibu wa Mradi wa barabara ya Goba – Madale (km 5), kutoka kampuni ya
Ujenzi ya Mwananchi Engineering and Contracting Co. Ltd (MECCO), Mhandisi Crispin
Mwombeki, amesema kuwa tayari wameshakamilisha usanifu wa mradi na
wanategemea kuanza kazi za Ujenzi hivi karibuni.
Utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya mradi wa Ujenzi wa barabara za kupunguza
msongamano katika jiji la Dar es salaam umeanza mwezi Desemba, mwaka 2016
ambapo umehusisha barabara tatu za Kifuru – Msigani (km 4.5), Goba – Makongo (km
4.5), na Goba – Madale (km 5) na kugharimu Jumla ya Shilingi Bilioni 24.2.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...