Na Oyuke Phostine
Makampuni ya bima nchini yametakiwa kusogeza hudama za bima ya Maisha kwa wanananchi ili kuchangia ukuajia wa uchumi wa nchi hususan katika kipindi hiki cha uchumi wa viwanda. Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji alipokuwa akifungua semina ya kimataifa ya Bima ya Maisha inayofanyika jijini Arusha.
Sekta ya bima nchini, kama ilivyo kwa mataifa mengine Afrika, inakumbwa na changamoto nyingi zikiwemo mwamko mdogo wa wananchi kununua bima, huduma kutofikia wananchi, na elimu ndogo ya masuala ya bima kuhusu bidhaa tofauti tofauti za bima.
“Tanzania tuna idadi ya watu takriba ni milioni hamsini, hili ni soko kubwa sana na fursa kwa makampuni ya bima kuwekeza, kwa maana hiyo mna deni la kuwafikia wananchi kwa kuwa na bidhaa za bima zenye ubunifu na zenye kutatua matatizo yao” amesema Dk. Kijaji.
Serikali imejidhatiti katika kuimarisha sekta ya bima kwa kuweka mipango madhubuti ya kuendeleza soko la bima kwa kurejesha imani ya wananchi juu ya huduma za bima zinazotolewa na makampuni yaliyosajiliwa nchini.
“Hili litachangia katika kuongeza ajira kwa vijana wa kitanzania, kwani ni lazima kisheria makampuni ya bima nchini kuwaajiri wazawa na tayari serikali ina vyuo vinavyotoa taaluma hii ya bima. Hivyo nina uhakika kuwa nguvu kazi yenye uweledi wa masuala ya bima inapatikana nchini” amesema Dk. Kijaji.
Pia Dk. Kijaji amitaka Mamlaka ya Bima nchi kupitia Kamishna wa Bima Nchini Dk. Baghayo Saqware kushirikiana na makampuni yenye usajili nchini kuhakikisha biashara ya bima inakuwa imara na yenye kunufaisha watanzania kwa sababu makampuni haya yanakusanya amana kutoka kwa watanzania.
Mkutano huo wenye dhima ya “Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Nini mchango wa bima ya maisha katika kuleta maendeleo endelevu” umewawezesha washiriki wote wa sekta ya bima kutoka Afrika na nje ya Afrika kujadili mada mbalimbali ili kuboresha soko la bima nchini na Afrika kwa ujumla.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...