NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni amempa maelekezo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuunda
Kamati ya kuchunguza uvamizi wa viwanja vya Gereza Isanga
uliofanywa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) mjini
Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi katika
Gereza hilo, Masauni alisema eneo hilo ambalo lina ukubwa wa ekari
zaidi ya 150 lazima lirudishwe katika himaya ya Jeshi la Magereza kama
lilivyokua awali.
“Eneo hili linalimilikiwa na Jeshi la Magereza tangu mwaka 1946,
haiwezekani watu watokee na kuchukua ardhi hii kiholelaholela, hii
haiwezekani hata kidogo, lazima uchunguzi ufanyike haraka
iwezekanavyo na eneo lote lilrudi mikononi mwa jeshi,” alisema
Masauni na kufafanua;
“Serikali ilishahamia hapa mjini Dodoma, hivyo shughuli za magereza
zitaongezeka kwa kasi, na umuhimu wa maeneo utakua mkubwa zaidi
kutokana na umuhimu wa jeshi hili katika kukuza uchumi.”
Aliongeza kuwa, jeshi hilo linahitaji kujenga nyumba za askari kwa kasi
na kutokana na changamoto hiyo ya uvamizi uliofanywa ujenzi waweza
kusuasua hivyo eneo hilo lahitajika kurudishwa haraka sana.
Masauni alifafanua kuwa, tayari amemuelekeza Katibu Mkuu wa wizara
hiyo, Meja Jenerali, Projest Rwegasira kulichunguza suala hilo kwa kina
kwa kuwa kuna taarifa ambazo bado hazijathibitishwa kuwa kati ya
wamiliki wa viwanja hivyo walikua ni viongozi waandamizi wa CDA,
Jeshi la Magereza pamoja na viongozi wakubwa mbalimbali.
Hata hivyo, Masauni alipiga marufuku mtu yeyote kuendeleza ujenzi wa
eneo hilo hata kama ana vibali vyote vya kumiliki eneo.
Aidha, Mkuu wa Gereza Isanga, Keneth Mwambeje, akizungumzia suala
hilo, alisema jeshi lake lina nyaraka za mawasiliano kati ya viongozi wa
gereza hilo ambao walikua kwa wakati huo pamoja na wa CDA.
CDA ambayo ilivunjwa na Rais John Magufuli, ndio inahusika kugawa
viwanja hivyo kwa wananchi zaidi ya mia moja ambao baadhi yao
wamejenga na wengine wanaendelea na ujenzi katika eneo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...