Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuanzisha chombo cha
kuendesha na kudhibiti sekta ndogo ya usafiri majini, usalama wa meli na mazingira ya
bahari ili kulinda maslahi mapana ya taifa.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame
Mbarawa wakati akijibu hoja ya Serikali kuhusu Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli
wa Taifa mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwenye
kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma.
Prof. Mbarawa amesema kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kupeleka Muswada
Bungeni wa kutunga sheria ambayo itaanzisha Shirika la Wakala wa Meli wa Taifa
(NASAC) ambao utasimamia usalama wa meli na bahari zetu kwa lengo la kuboresha
utendaji kazi wa bandari zetu kama mnavyojua bandarini kumekuwa na changamoto
nyingi. “Hivi karibuni tumeshuhudia upotevu wa mali na vitu vingi pale bandarini kama
vile madini na vitu vingine vinaingia bila utaratibu,” amefafanua Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa Serikali imeona ibadilishe mtazamo uliokuwepo zamani kupitia
SUMATRA ambayo inasimamia masuala ya nchi kavu na majini, “Serikali imeona
ianzishe chombo kingine ili kiweze kujikita kusamimia masuala ya usafiri wa majini
pekee na masuala nyeti hasa ya uchumi wetu kama vile madini”. Chombo kimoja cha
kutoa huduma na kudhibiti sio jambo geni.
Hapa nchini tunayo taasisi ya Mamlaka ya
Anga Tanzania (TCAA) ambayo inatoa huduma ya anga na kudhibiti anga, hivyo
Serikali inataka kufanya hivyo pia kwenye sekta ya usafiri wa majini. Hili si jambo geni
kwa kuwa linafanyika kwenye nchi nyingine kama vile ya bandari ya Singapore na nchi
nyingine ya India.
Aidha, Prof. Mbarawa ametoa wito kwa wadau kushirikiana na Serikali kuanzisha
chombo hiki. Pia amefafanua kuwa SUMATRA haitapokonywa majukumu yake bali nia
ya Serikali ni kuitaka SUMATRA isimamie sekta ya nchi kavu tu kwa maana ya
barabara, reli, magari ambayo ni sehemu kubwa na ina changamoto ambayo inahitajika
kutatuliwa hivyo ijikite huko na sekta hii ndogo ya usafiri wa majini iwe na chombo
kingine tofauti ili sheria iweze kutusaidia kukuza uchumi wa baharini na wa nchi kavu.
Ni imani ya Serikali kuwa, kwa kuwa na chombo cha udhabiti cha sekta ya nchi kavu
ambapo NASAC itaanzishwa kwa ajili ya sekta ya usafiri wa majini, utaziwezesha sekta
hizi za majini na nchi kavu kukua vizuri hivyo kukuza uchumi wetu, watanzania
watapata ajira na kampuni nyingi za meli zitaingia nchini na kufanya kazi kwa kuwa
mahali ambapo hakuna udhibiti sekta haiwezi kukua, “angalieni sekta nyingine kama ya
mawasiliano ambako kuna udhibiti mzuri na sekta inakua vizuri” amesema Prof.
Mbarawa. Kwa mantiki hiyo, Serikali itawasilisha sheria ya SUMATRA Bungeni ili
kufanyiwa maboresho ili iweze kuchangia vizuri ukuaji wa sekta ya nchi kavu na iende
na wakati.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu
Prof. Norman Sigalla King amesema kuwa azma ya Serikali ni nzuri katika muendelezo
wa kuhakikisha kuwa taasisi zinazoanzishwa zina mgusa mlaji na kwa manufaa ya
Serikali kwa ujumla. Serikali imejibu hoja zote za wadau na Kamati yetu inaendelea
kuchambua hoja hizo ili kuhakikisha kuwa inasimamia na kuishauri Serikali kwenye
Muswada huu.
Ni dhamira ya Kamati kuona kuwa biashara bandarini inaendelea
kuimarishwa na kudhibitiwa; na nchi yetu sio pekee yenye bandari kwenye ukanda huu
hivyo ni lengo la Kamati kuhakikisha kuwa Muswada huu unaopendekezwa
unaboreshwa ili kuhakikisha una akisi ushindani. Ameongeza kuwa Rais wetu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameelekeza udhibiti
kwenye bandari yetu, hivyo huu ni mlolongo wa kusimamia na kudhibiti shughuli za
uendeshaji wa bandari.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...