Anaandika Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)mkoani Kilimanjaro,imemtia mbaroni Daktari wa Hospital ya rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi akituhumiwa kudai na kupokea rushwa ya shilingi 150,000.
Daktari huyo,Deogratias Godfrey Urio,alikamatwa jana katika mji mdogo wa Himo kwenye baa maarufu ya Mombasa High Way baada ya kuwekewa mtego na makachero wa takukuru mkoani Kilimanjaro.
Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro(RBC),Holle Makungu imesema kuwa kukamatwa kwa daktari huyo kunatokana na malalamiko ya ndugu wa mgonjwa aliyekuwa akipigwa dana dana kupatiwa huduma ya upasuaji katika hospital hiyo.
Makungu ameeleza katika taarifa yake kuwa,mgonjwa huyo alikuwa akihitaji kufanyiwa upasuaji wa uvimbe katika kizazi chake tangu oktoba mwaka huu baada ya kufanyiwa vipimo kwenye hospital hiyo na kubainika kuwepo kwa uvimbe.
Lakini licha ya kubainika kuwepo na uvimbe huo,mgonjwa huyo hakuweza kupata tiba haraka baada ya kuelezwa na daktari huyo kuwa hawezi kufanyiwa upasuaji huo hadi hapo atakapotoa fedha hizo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...