Watalaam wa Masuala ya Nishati wakifuatilia taarifa kuhusu masuala ya umeme wakati wa Mkutano wa
12 wa Baraza la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Asteria Muhozya, Arusha
Wataalam wa Masuala ya Nishati wanaoshiriki Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Jumuiya ya Afrika
Mashariki unaondelea jijini Arusha wameibua masuala kadhaa katika mkutano huo ambayo yanalenga
kuharakisha utekelezaji wa miradi ya Nishati iliyokubaliwa na Jumuiya hiyo.
Hayo yalibainika katika siku ya Pili ya mkutano wa Timu ya Wataalam kutoka Jumuiya hiyo ulioanza
tarehe 30 Oktoba, 2017. Mkutano wa Wataalam umefanyika kabla ya kikao cha Makatibu Wakuu
kitakachofanyika tarehe 2 Oktoba, 2017 na kitafuatiwa na kikao cha Mawaziri wa Nishati
kinachotarajiwa kuhitimisha mkutano huo tarehe 3 Oktoba,2017.
Baadhi ya miradi ya umeme iliyojadiliwa ni pamoja na ile ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha
Umeme inayounganisha nchi na nchi ambayo imeelezwa kuwa na kasi ndogo katika utekelezaji wake.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa Miundombinu ya Kusafirisha Umeme wa Msongo
wa kV 400 wa Singida- Arusha- Namanga, mradi wa kV 220 wa Rusumo- Nyakanazi na mradi wa kV 400
wa Iringa- Mbeya - Tunduma.
Pia, Wataalam hao wamejadili masuala ya kodi kwa vifaa vya umeme jua, miradi ya umeme ya mipakani
ikiwemo miradi ya Murongo/Kigagati na Nsogezi pamoja na Sera ya Usalama wa Nishati ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Baadhi ya Wataalam kutoka Tanzania wakijadiliana jambo wakati wa mkutano huo.
Aidha, katika siku mbili za majadiliano, Watalaam kutoka Jumuiya hiyo pia wamejadili masuala kadhaa
yakiwemo yanayohusu nishati jadidifu, gesi asilia na mafuta.
Kikao cha Makatibu Wakuu, kitakachofanyika tarehe 2 Oktoba, kitatanguliwa na kikao cha Kamati ya
Nishati cha Baraza hilo kinachofanyika leo tarehe 1 Oktoba, 2017 ambapo hoja mbalimbali zilizoibuliwa
na Wataalam hao zitajadiliwa katika kikao hicho.
Awali, akifungua mkutano wa Baraza hilo kwa upande wa Wataalam tarehe 30 Oktoba, 2017 Naibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki upande wa Sekta za Kijamii na Uzalishaji, Christophe
Bazivamo alieleza umuhimu wa nchi husika kuongeza kasi ya upatikanaji wa Nishati miongoni mwa nchi
wananchama ili kuwezesha mapinduzi ya Viwanda na kusisitiza kuwa, miongoni mwa maeneo ya
kipaumbele ya Jumuiya hiyo ni Nishati.
Wataalam kutoka nchi mbalimbali wakijadiliana kuhusu masuala ya mafuta na gesi asilia wakati wa Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Bazivamo aliongeza kuwa, ili nchi hizo ziendeleee kiviwanda zinahitaji nishati kwa kuwa ndiyo kichocheo
kikuu cha maendeleo na kwamba, bado idadi kubwa ya wananchi wa jumuiya hiyo haijaunganishwa na
nishati ya umeme.
Pia, aliongeza kuwa, ukosefu wa nishati hiyo siyo tu unadidimiza maendeleo ya watu pia unaathiri sekta
ya elimu kwa kuwa, kukosekana na nishati kunasababisha wanafunzi hususani waishio vijijini kutumia
muda mwingi kutafuta nishati ya kuni kwa ajili ya kupikia badala ya kujikita na masomo.
Nchi zinazoshiriki mkutano huo ni pamoja na Tanzania, Uganda, Rwanda, Uganda na Kenya. Aidha,
Tanzania inawakilishwa na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji, Mazingira na
Nishati ya Zanzibar, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Wakala wa Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu
wa Mafuta , Zanzibar (ZURA). Mwenyekiti wa Mkutano wa 12 wa Baraza hilo ni nchi ya Uganda na Katibu ni nchi ya Rwanda.
Baadhi ya Wataalam kutoka nchini Kenya wakijadiliana jambo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...