WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wana-Lindi na wana-Ruangwa watumie fursa zilizopo ili kufanikisha maandalizi ya sherehe za Maulid na Baraza la Maulid Kitaifa mwaka huu.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Novemba 5, 2017) wakati akizungumza na viongozi wa dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Lindi na wilaya ya Ruangwa mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja.
Waziri Mkuu amesema sherehe hizo zitafanyika Desemba mosi kwa mkesha wa Maulid na kufuatiwa na Baraza la Maulid litakalofanyika Desemba 2, saa 3 asubuhi kwenye viwanja vya shule ya msingi Likangale.
Aliwataka wana-Ruangwa waharakishe kujenga nyumba za kulala wageni na sehemu za kula ili waweze kupokea ugeni huo mkubwa wa kitaifa. “Kila mmoja anayeona hapo kuna fursa, ni lazima aitumie vizuri,” alisisitiza.
“Kwa niaba ya wana-Ruangwa, tunamshukuru Mheshimiwa Mufti na Baraza la Maulamaa kwa kuridhia sherehe hizi zifanyike kitaifa hapa wilayani kwetu. Nitumie fursa hii kuwaomba Waislamu wote tuungane katika sherehe hizi licha ya tofauti za madhehebu yetu tuliyonayo,” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...