Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu (kati kati), akiwatoa hofu Watendaji wa
Mamalaka ya Vitambulisho vya TAifa (NIDA) kwamba kuanzia mwezi January 2018, Idara ya Uhamiaji
Zanzbar imejipanga kushughulikia maombi ya Vitambulisho vya Taifa kwa Raia wote watakaofika
katika Ofisi yao iliyopo Kinduni, Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja, badala ya kufuata huduma Ofisi ya
Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini iliyopo Kivunge. Hatua hiyo ni utekelezaji wa Ahadi za Serikali kufikisha
huduma karibu na Wananchi. Aliyasema hayo wakati alipotembelea Ofisi hizo wakati wa ziara ya
kikazi katika Wilayani humo tarehe 05 - 06 Disemba, 2017.
Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu, amewapongeza
watendaji wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwa kusogeza huduma za
Uhamiaji karibu na Jamii inayowazunguka. Alitoa pongezi hizo leo alipotembelea Vituo
Maalum “Detached Points” vilivyopo ndani ya maeneo ya Kendwa na Nungwi, Shehia za
Nungwi - Banda Kuu, Mnarani na Kiungani, Wilaya ya Kaskazini “A” na Fukwe za
Kiwengwa, Pongwe na Pwani mchangani, Shehia za Kiwengwa, Moga na Pongwe kwa
Wilaya ya Kaskazini “B” alipofanya ziara ya kikazi katika Wilayani hizo tarehe 05 – 06
Disemba, 2017.
Mkoa wa Kaskazini Unguja ni kitovu cha shughuli za Biashara na Uwekezaji katika sekta
ya Utalii, hali inayosababisha kuwavuta wageni wengi kutoka Mataifa mbali mbali
Duniani kutembelea maeneo hayo kwa madhumuni tofauti. “katika Mkoa huu Idara yetu
ina kazi kubwa ya kuhudumia wageni wanaoingia na kuishi ndani ya Mkoa huu, kwani ni
Mkoa ambao huwavuta wageni wanaokuja kutembea na kupumzika kwenye fukwe
nadhifu, kuna wanaokuja kwa kuwekeza na wale wanaokuja kufanyakazi na biashara
mbali mbali za Utalii, hali ambayo huibua changamoto nyingi za Kiuhamiaji” alisema
Kamishna Sururu.
Kutokana na muingiliano huo wa wageni wa makundi tofauti, Idara ya Uhamiaji yenye
dhamana ya kuhakikisha wageni wote wanaoingia na kuishi nchini wanafanya hivyo kwa
mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Uhamiaji, ina mchango mkubwa katika
kuimarisha Ulinzi, Uchumi na Utamaduni wa watu wa Zanzibar. Kuanzishwa kwa Vituo
maalum kwenye maeneo hayo ni mapinduzi makubwa katika Udhibiti na Usimamizi wa
wageni wanaoingia na kuishi Zanzibar kinyume cha Sheria.
“Kwa kweli Nimefarijika sana kuona jinsi mlivyojipanga kuweza kuyafikia maeneo yote
yenye changamoto za uwepo wa baadhi ya wageni wanaojipenyeza na kuishi nchini bila
ya Kufuata Sheria za Uhamiaji. Uwepo wa Vituo hivi naamini ni muarobaini wa kuondoa
kabisa tatizo la Uhamiaji haramu” Alisema Kamishna Sururu na kuongeza “Hatuzuwii
wageni kuja kutembea, hatuzuwii wageni kufanyakazi ama kuwekeza nchini kwetu bali
tunataka wageni wote waingie na kuishi nchini kwa kuheshimu Sheria za Nchi yetu, kwa
kufanya hivyo tutaweza kufikia ile adhma njema ya serikali kufungua milango ya
Biashara na Uwekezaji katika sekta ya Utalii kwa manufaa makubwa bila ya kuathiri
Jamii na Tamaduni zetu”.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...