Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. A. P. Makakala ametoa salaam za Heri ya Sikukuu ya Uhuru wa Tanzania bara kwa Watanzania alipokuwa akiwaaga watumishi wa Idara ya Uhamiaji Makao Makuu akielekea Mkoani Dodoma kuhudhuria maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania bara.
Akizungumza Ofisini kwake Kamishna huyo amewataka Watanzania kudumisha uzalendo kwa kulinda Rasilimali, Ulinzi na Usalama wa nchi kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho. Hii ikiwa ndio njia pekee ya kuwaenzi waasisi wa Taifa letu.
“Uraia wetu una umuhimu wa kipekee kwani umebaki kuwa ndio msingi na utambulisho wetu unaotaunganisha wananchi wote bila ya ubaguzi ukilinganisha na utambulisho mwingine kama ukabila au dini na ndio utambulisho wetu kimataifa.Taifa lolote huru liwe kubwa au dogo haliwezi kukamilika bila ya kuwa na raia wake, ndiyo maana miaka 56 ya Uhuru wetu tunajitambua na kujivunia kuwa Watanzania” Alisema Kamishna Jenerali wa Uhamiaji.
Kwa msingi huo suala la kutambua nani ni raia na nani ni mgeni litabakia kuwa lengo kuu la Idara, kwakuwa raia ndiyo wanaotakiwa kunufaika na Rasilimali za nchi na Haki zinazotolewa na nchi kwa raia wake.
Pamoja na haki hizo za Kikatiba na za asili, lakini pia ni raia hao wenye wajibu wa kulinda Taifa lao dhidi ya uvamizi wowote na rasilimali za Taifa kama zilivyopiganiwa na Mwasisi na Baba wa Taifa letu Hayati Mwl Julius K. Nyerere na kuongeza kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa nchi ni la wananchi wote na hasa wazalendo.
Ni vyema kufahamu kuwa Uraia wetu ndio Utanzania wetu hivyo basi hatuna budi kuadhimisha siku hii adhimu tukiwa na ndoto na matarajio ya kuijenga Tanzania mpya ya Viwanda.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...