Timu ya soka ya waandishi wa habari za michezo nchini (Taswa SC) kesho itacheza mechi maalum ya kirafiki dhidi ya timu ya Saleni FC kwenye uwanja wa Saleni, Lugoba.
Mechi hiyo imepangwa kuanza saa 10.00 jioni na imeandaliwa kwa lengo la kudumisha ushirikiano baina ya timu hizo mbili.
Mwenyekiti wa Taswa SC Majuto Omary alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na timu ya waandishi itaondoka jijini saa 3.00 kuelekea Lugoba, Chalinze.
Majuto alisema kuwa wachezaji wote wa Taswa SC wanatakiwa kuwahi kufika ili kuondoka mapema na kuwahi shughuli nyingine zilizoandaliwa na wakazi wa Saleni kabla ya kuanza kwa mechi hiyo.
Alisema kuwa wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo ambao mbali ya kudumisha ushirikiano, pia utatumika kuangalia vipaji mbalimbali vya wachezaji wanaoishi katika eneo hilo.
“Tumejiandaa vizuri sana, na kudhihirisha hilo, tumeshinda mechi mbili mfululizo dhidi ya timu ya Polisi Kombaini ambao tuliwafunga mabao 5-0 na juzi tu tumewafunga Wabunge wa Jamhuri ya Muungano waTanzania (Bunge SC) mabao 4-2, kwa kifupi tupo vizuri sana,” alisema Majuto.
Alifafanua kuwa baada ya mechi hiyo, timu yao itaendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Shule ya Kisasa ya Kenton iliyopo Sinza Afrika Sana kwa maandalizi ya mechi na safari nyingine za nje ya mkoa.
Alisema kuwa Taswa SC Jumapili inatarajia kucheza mechi nyingine ya dhidi ya timu ya Kijitonyama Chipukizi Veterans, mchezo ambao umepangwa kufanyika kwenye uwanja wa Bora, Kijitonyama.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...