Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini wamesisitizwa kujiunga kwenye vikundi ili iwe
rahisi kusaidiwa.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametoa wito huo hivi karibuni Wilayani
Ruangwa Mkoani Lindi, kwenye mkutano wake na Wachimbaji Wadogo wa Madini
ya Dhahabu na Vito (Green Garnet) wa Namungo wilayani humo.
Nyongo alisema dhamira ya Serikali ni kuwasaidia wachimbaji wadogo kuwa na
uchimbaji wenye manufaa kwao na Taifa kwa ujumla na ili kufikia dhamira hiyo ni
vyema wakajiunga kwenye vikundi.
"Mkijiunga kwenye vikundi itakua ni rahisi kuwafikia kwa pamoja na kuwapatia
misaada mbalimbali yenye tija kwenye shughuli zenu," alisema.
Alisisitiza kwamba umoja ni nguvu, na ili mchimbaji awe na uwezo na nguvu kwenye
utekelezaji wa majukumu yake inabidi afanye kazi akiwa ndani ya umoja na
wenzake.
Alisema pale ambapo wachimbaji watakua wamejiunga kwenye vikundi, itakua rahisi
hata kwa Taasisi za kifedha kuweza kuwafikia na kuwasaidia ikiwemo kuwapatia
elimu ya fedha na vilevile mikopo.
"Nimekuja hapa kuzungumza nanyi ili kubaini changamoto zinazowakabili kwa ajili
ya kuzitafutia ufumbuzi, na pia ninawaasa mhakikishe mnajiunga kwenye vikundi,"
alisema.
Aliongeza kwamba Serikali ingependa kuona Wachimbaji Wadogo wa Madini
wanafanikiwa kufikia kwenye uchimbaji wa Kati na baadaye kuwa Wachimbaji
Wakubwa.
Aidha, Wachimbaji hao walimuomba Naibu Waziri Nyongo kuendelea kuwatembelea
mara kwa mara ili kuelewa changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi kila
inapobidi.
Baada ya kuzungumza na wachimbaji hao, Naibu Waziri Nyongo alitembelea Mgodi
wa Dhahabu unaomilikiwa na Kampuni ya Germin Exploration ya Namungo huko
Ruangwa na kukagua shughuli zinazofanywa na mgodi huo.
Vilevile alitembelea mradi wa kuchimba Madini ya Kinywe (Graphite) wa Kampuni ya
PACCO GEMS LTD iliyopo katika vijiji vya Mtondo na Nanjaru wilayani humo
ambapo aliahidi kuwasaidia kumaliza tatizo la upatikanaji wa hati ya umiliki wa ardhi
wanayohitaji ili mradi uweze kuanza mara moja.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akizungumza alipotembelea
Mgodi unaomilikiwa na Kampuni ya Germin Exploration.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akipata maelezo ya Mradi wa
kuchimba Madini ya Kinywe (Graphite) wa Kampuni ya PACCO GEMS LTD iliyopo
katika kijiji cha Mtondo na Nanjaru wilayani humo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alipotembelea na kuzungumza na
Wachimbaji kwenye Miradi ya kuchimba Madini ya Dhahabu na Kinywe Wilayani
Ruangwa.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akipata maelezo ya Mradi wa
kuchimba Madini ya Kinywe (Graphite) wa Kampuni ya PACCO GEMS LTD iliyopo
katika kijiji cha Mtondo na Nanjaru wilayani humo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...