Wizara ya Madini kupitia Kitengo cha Mazingira kwa kushirikiana na
Taasisi ya Kimataifa kutoka nchini Canada (CIRDI) wameanza kutoa
mafunzo ya ufungaji wa migodi kwa wataalam kutoka Taasisi za Serikali
zinazosimamia Sekta ya Madini ndani na nje ya nchi. Mkuu wa Kitengo cha Mazingira katika Wizara ya Madini, Gidion Kasege
amesema kuwa wataalam hao watapata mafunzo kuhusu ukokotoaji wa
mahesabu ya gharama za ufungaji migodi, usimamizi wa maji migodini na
jinsi ya kutengeneza sehemu ya kuhifadhia mabaki ya uchenjuaji (mining
tailings).
Alisema kuwa, hii ni mara ya pili kwa Taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa
wataalam hao wa Madini na kwamba Awamu hii imeshiriksha nchi nyingine
za Afrika ili wataalam hao waweze kubadilishana uzoefu na kujifunza
mafanikio na changamoto ambazo nchi hizo zinapata katika shughuli za
ufungaji wa migodi. Alieleza kuwa nchi zinazohudhuria mafunzo hayo ni Tanzania, Kenya,
Namibia na Ethiopia, ambapo mafunzo yanatolewa kwa njia ya nadharia na
vitendo katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na Buzwagi uliopo
mkoani Shinyanga.
Naye, Afisa katika Ofisi ya Madini mkoani Shinyanga, Mhandisi Joseph
Kumburu ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo wataalam wataongeza
uelewa katika shughuli za usimamizi wa migodi nchini na hivyo kuhakikisha
kuwa migodi inafuata taratibu zote zinazotakiwa wakati wa usitishaji wa
shughuli zao nchini. Alisema kuwa kupitia changamoto ambazo nchi nyingine wamepata katika
shughuli hizo za madini, itawasaidia kuwa makini zaidi wa utekelezaji wa
shughuli hizo nchini.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira kutoka Wizara ya Madini, Innocent
Makomba, alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa wataalam kwani
yanaongeza uelewa wa masuala yanayopaswa kutekelezwa kabla ya
ufungaji wa migodi ikiwemo suala la kushirikisha jamii inayozunguka migodi
kabla ya kufanyika kwa maamuzi.
" Tunajifunza kuwa ni muhimu kushirikisha jamii kwani wao wanaweza
kuamua kuwa maeneo ambayo uchimbaji umeshafanyika yatengenezwe
kwa ajili ya kufanyia shughuli nyingine kama uvuvi, kilimo au hata kuwa
makazi ya watu na kupitia mafunzo haya tumeona mifano ya jinsi nchi
nyingine zilivyotekeleza suala hilo," alisema Makomba.
Vilevile, Makomba alisema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea uelewa
katika suala utengenezaji wa sehemu za kuhifadhia mabaki ya uchenjuaji
(mining tailings) ili zisilete madhara kwa wananchi au mazingira.
Wataalam wa Madini kutoka Tanzania na Ethiopia wakifuatilia
mafunzo ya ufungaji migodi yaliyokuwa yanatolewa na wakufunzi
kutoka Taasisi ya Kimataifa ya nchini Canada (CIRDI).
Mkufunzi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya nchini Canada (CIRDI),
Colleen Crystal akitoa mafunzo kuhusu uhifadhi wa mabaki ya
uchenjuaji (mining tailings) kwa wataalam wa Madini wa Tanzania na
nje ya Tanzania.
Wataalam wa Madini kutoka nchini Tanzania wakifuatilia mafunzo
ya ufungaji migodi yaliyokuwa yanatolewa na wakufunzi kutoka
Taasisi ya Kimataifa ya nchini Canada (CIRDI).
Wataalam wa Madini kutoka ndani na nje ya nchi wakiwa katika
mafunzo ya ufungaji migodi yaliyoratibiwa na Wizara ya Madini na
Taasisi ya Kimataifa kutoka nchini Canada (CIRDI).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...