Na Oliver Njunwa- Dar es Salaam

Chuo cha Kodi (ITA) pamoja na Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB), vimeingia katika makubaliano ya kushirikiana katika kuwajengea uwezo Mawakala wa Forodha Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya hafla fupi ya kutiliana saini makubaliano hayo, iliyofanyika hivi karibuni katika Chuo cha Kodi jijini Dar es salaam, Mkuu wa Chuo hicho Prof. Isaya Jairo amesema kwamba, makubaliano hayo ni muhimu kwani kila upande una watalaam wa kutosha kuwasaidia Mawakala wa Forodha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“ITA inajivunia utaalam wake wa kufundisha na ZFB ina utaalamu katika masuala ya kiforodha. Kwa hiyo wote kwa pamoja tutashirikiana ili malengo ya makubaliano haya yaweze kufikiwa”, alisema Prof. Jairo.

Prof. Jairo aliongeza kuwa, katika makubaliano hayo, Chuo cha Kodi kitatoa mafunzo ya muda mfupi na utaalamu wa masuala ya forodha kwa ZFB ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na Mawakala wa Forodha wanaofanya kazi kwa weledi.

Mkuu wa Chuo cha Kodi pia amesema kwamba lengo la vyuo sio kupata fedha bali kutoa wataalamu wa kutosha ambapo uwezo wa Chuo hupimwa kwa idadi ya wanafunzi wanaohitimu na aina ya sifa walizonazo.

Aidha, Prof. Jairo ameiomba ZFB kulinda hadhi ya jina la Chuo cha Kodi kwani kina jina zuri kutokana na uzoefu wake wa kutekeleza makubaliano ya ushirikiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB) Omar Hussein Mussa wakibadilishana hati za makubaliano ya ushirikiano katika kuwajengea uwezo wanachama wa ZFB.
Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar Omar Hussein Mussa wakizungumza na wajumbe wa Kamati ya Makubaliano kutoka Chuo cha Kodi (Kulia) na Zanzibar (kushoto) kabla ya kusaini hati za makubaliano katika chumba cha mikutano ITA.
Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (wa pili kushoto), Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB) Omar Hussein Mussa (wa pili Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala Tanzania (TAFFA) Stephen Ngatunga (wa kwanza kulia) katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya ushirikiano mara baada ya kusaini makubaliano ya kuwajengea uwezo mawakala wa Forodha Zanzibar. (PICHA ZOTE NA OLIVER NJUNWA).



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...