Na Mwandishi Wetu, Moshi.
MFANYABIASHARA na mzaliwa wa Kijiji cha Uchau Kaskazini wilaya ya Moshi Vijijini, Emmanuel Mallya, ameikabidhi serikali zahanati ikiwa na vifaa vya kisasa vikiwamo vitanda vya wagonjwa vinavyotumia nishati ya umeme.
Zahanati hiyo inayojukana kwa jina la EB zahanati, imejengwa na mfanyabiashara huyo kwa kutumia nguvu zake mwenyewe bila kuhusisha msaada kutoka Halmashauri ya wilaya ya Moshi wala serikali kuu.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuikabidhi zahanati hiyo kwa serikali, mfanyabiashara huyo alisema wazo la kujenga zahanati hiyo lilitokana na kuwepo na changamoto za umbali wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
Alisema changamoto hiyo ilipelekea kuwepo na vifo vya watu wengi vilivyochangiwa na umbali wa upatikanaji wa vituo vya afya na kwamba changamoto hizo ndizo zilizomsukama kuona haja ya kujenga zahanati hiyo.
Alitoa wito kwa mamlaka husika kuitunza zahanati hiyo pamoja na vifaa vitakavyotumika katika kuwahudumia wagonjwa huku akitoa wito kwa watu wengine wenye uwezo kujitolea katika kuwahudumia wananchi wasio nacho.
“Utajiri unatokana na moyo wa mtu alionao, unaweza ukawa na utajiri na usiwe na moyo wa kuwasaidia wengine, kila mtu amepewa karama na mwenyezi Mungu, muhimu hapa ni namna ya kuzitambua hizo karama,” alisema.
Mfanyabiashara, Emmanuel Mallya (katikati) akisaini hati na mkataba wa zahanati EB, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Michael Kilawila kwenye hafla hiyo ya makabidhiano. Kushoto ni mke wa Bw. Mallya, Bi. Marry Mallya akishuhudia makabidhiano hayo.

Mfanyabiashara, Emmanuel Mallya (kushoto) akimkabidhi hati na mkataba wa zahanati EB Zahanati Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Michael Kilawila kwenye hafla hiyo ya makabidhiano.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...