Na Ramadhani Juma, Ofisi ya Mkurugenzi .
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 2.1 kwa ajili ya kukarabati Shule za Sekondari za Bihawana na Dodoma zilizopo Manispaa ya Dodoma ikiwa ni sehemu ya utekezaji wa mpango wa Serikali wa kuzifanyia ukarabati mkubwa Shule kongwe Nchini.
Kati ya Fedha hizo, zaidi ya Shilingi Bilioni 1.2 zitatumika kukarabati Shule ya Sekondari ya Bihawana pekee na zaidi ya Shilingi Milioni 900 zitatumika katika Shule ya Sekondari ya Dodoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kazi ya ukarabati katika shule hizo jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TEA Graceana Shirima alisema kuwa, shughuli ya ukarabati ilitanguliwa na upembuzi yakinifu wa hali halisi ya mahitaji ya ukarabati uliofanywa na mtaalamu mshauri ambaye ni Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
“Baada ya upembuzi yakinifu, maeneo ya kipaumbele katika ukarabati kwa awamu hii itahusisha Madarasa, maabara, bwalo na jiko, vyoo, na mifumo ya umeme, mifumo ya TEHAMA na mifumo na maji safi na maji taka” alisema Shirima.
Alisema awamu hii ya ukarabati inatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi minne, na awamu nyingine za ukarabati zitatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Graceana Shirima
(wa pili kushoto) akikagua shughuli ya ukarabati katika Shule ya
Sekondari ya Dodoma baada ya kuzindua rasmi kazi hiyo. TEA imetoa zaidi
ya Shilingi milioni 900 kwa ajili ya ukarabati huo. Kushoto ni
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi na kulia ni Mhandisi
Lupakisyo Mwalwiba ambaye ni Meneja Miradi kutoka Chuo cha Sayansi na
Teknolojia Mbeya (MUST) ambaye ndiyo Mtaalamu Mshauri.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TEA Graceana Shirima (kushoto) akikagua maeneo
mbalimbali yanayofanyiwa ukarabati katika Shule ya Sekondari ya Bihawana
iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma jana mara baada ya kufanya
uzinduzi rasmi wa kazi hiyo. TEA imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.2
kwa ajili ya kuikarabati Shule hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...