WANANCHI wa Kitongoji cha Mahiga, Kijiji cha Mwakitolyo, Tarafa ya Nindo Wilayani Shinyanga wametakiwa kufanya subira wakati mgogoro wao wa fidia na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya uchimbaji madini ya Henan Afro Asian Engineering ukitafutiwa ufumbuzi.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ametoa wito huo Machi 12, 2018 kwenye mkutano na wananchi hao uliofanyikia kwenye Kitongoji cha Mahiga na kuhudhuriwa na watendaji mbalimbali wa Serikali.
Mkutano huo unafuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alilolitoa Machi 11, 2018 kwenye mkutano na wananchi wa Kahama ambapo alielezwa na Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum kuwa wananchi wa Mahiga wana mgogoro wa muda mrefu na mwekezaji hususan kuhusiana na suala la ulipaji fidia ili kupisha mradi.
Kufuatia maelezo hayo ya Mbunge, Rais Dkt. Magufuli alimuagiza Naibu Waziri Biteko kuhakikisha anafika kwenye eneo hilo ili kujionea hali halisi na kuwasikiliza wananchi.
Rais Magufuli alisisitiza kuwa ni wakati sasa Watanzania waanze kunufaika na rasilimali zao ikiwemo madini. "Tunataka madini yawanufaishe Watanzania," alisema Rais Magufuli.Alisema wawekezaji wakifika nchini ni lazima wahakikishe Watanzania wananufaika kwa namna mbalimbali ikiwemo ajira, kodi na tozo.
"Jukumu langu nimeamua kusimamia suala hili; Nawahakikishia Serikali iko imara kwa ajili ya kuwatetea wanyonge," alisema Rais Dkt. Magufuli.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Mahiga, Kijiji cha Mwakitolyo Wilayani Shinyanga (hawapo pichani) kuhusu mgogoro wao na Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Henan Afro Asian Engineering.
Wananchi wa Kijiji cha Mwakitolyo, Wilayani Shinyanga wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) akizungumza kuhusu mgogoro wao na Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Henan Afro Asian Engineering.
Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum akizungumza na wananchi wake wa Kitongoji cha Mahiga, Kijiji cha Mwakitolyo, Tarafa ya Nindo Wilayani Shinyanga kuhusiana na mgogoro wao na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Henan Afro Asian Engineering.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...