Na Grace Michael, Morogoro
KATIKA kuhakikisha Watanzania wanakuwa na uhakika wa kupata huduma
za matibabu kupitia Mfumo wa Bima ya Afya, Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya umekutana na waratibu wake kutoka halmashauri zote nchini kwa
lengo la kujipanga kuwafikia wananchi wengi zaidi pamoja na uboreshaji
wa huduma kwa wanachama.
Akifungua kikao kazi hicho cha siku mbili, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF,
Bernard Konga alisema kuwa ili kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya
Tano ya Serikali ya Viwanda ni lazima Mfuko kwa kushirikiana na wadau
wake kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa kwa kujiunga na Mfuko
ili kuwa na uhakika wa huduma za matibabu.
“Ili kufikia lengo la Nchi ya Viwanda ambalo Rais wetu amelianzisha, ni
lazima tuhakikishe wananchi wote wanakuwa na uhakika wa kupata
huduma za matibabu wakati wanapopatwa na magonjwa na ndio maana
tumeamua kabisa tukutane kwa pamoja ili tukubaliane namna bora ya
kuwafikia lakini pia kuboresha na kuimarisha huduma za matibabu katika
vituo vya kutolea huduma,” alisema Bw. Konga.
Kikao hicho pia kina lengo la kupata mrejesho wa pande zote mbili kuhusu
maboresho mbalimbali yaliyofanyika ndani ya Mfuko na kujadili kwa
pamoja mambo yanayohitaji kuboreshwa kwa lengo la kuongeza wigo na
kutoa huduma bora.
Mkurugenzi Mkuu pia alisisitiza juu ya kukabiliana na tatizo la udanganyifu
ambalo limekuwa likifanywa na baadhi ya watoa huduma wasiokuwa
waaminifu hali inayorudisha nyuma jitihada kubwa za Mfuko za kuimarisha
Mfuko.
Alisema kuwa kwa upande wa Mfuko, umeanzisha mifumo mbalimbali ya
TEHAMA ambayo inatumika katika kubana mianya ya udanganyifu kwenye
utumiaji wa huduma na uwasilishaji wa madai ya watoa huduma hivyo akawaomba waratibu hao kutoa ushirikiano mkubwa katika suala hili kwa
lengo la kulinda uhai wa Mfuko.
Kwa upande wa waratibu wamesema kuwa mkutano huo ni fursa kubwa
kwao kupata taarifa mbalimbali za maboresho yaliyofanywa na kujengeana
uwezo wa ushawishi kwa wananchi kujiunga na huduma za Mfuko.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw. Bernad Konga akifungua kikao kazi kilichohusisha Waratibu wa Mfuko kutoka Halmashauri zote nchini mjini Morogoro.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Bw. Bernard Konga akifuatilia mada zilizokuwa zinawasilishwa katikati ni Meneja wa NHIF, Mkoa wa Morogoro Bi. Agnes Chaki na Kushoto ni Mkurugenzi wa
Utawala na Rasilimali Watu Bw. Charles Lengeju.
Waratibu wa Mfuko wakifuatilia mada mbalimbali kutoka kwa wawezeshaji






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...