Na Teresia Mhagama
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amesema kuwa, baada ya miezi mitatu Serikali itatoa uamuzi kama nchi iendelee kutumia mita za umeme zinazotengenezwa nje ya nchi au kupiga marufuku uingizaji wa mita hizo baada ya kujiridhisha na uwezo wa viwanda vya ndani katika kuzalisha mita husika.
Dkt. Kalemani ameyasema hayo jijini Dar es Salam tarehe 23 Machi, 2018 wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha Baobab Energy Systems kinachozalisha mita za umeme lengo likiwa ni kujiridhisha na uwezo wa kiwanda hicho katika kukidhi mahitaji ya mita nchini.
"Serikali imeweka miezi mitatu ya matazamio ili kuona kama viwanda vyetu ambavyo sasa ni viwili, vina uwezo wa kuzalisha mita za umeme za kutosha na zenye ubora zitakazokidhi soko la ndani kisha tutatoa uamuzi kuhusu uingizaji wa mita hizo nchini," alisema Dkt. Kalemani.
" Miezi kadhaa iliyopita Serikali ilitoa katazo la kuagiza nguzo za umeme na transfoma kutoka nje ya nchi, baada ya kujiridhisha kuwa uwezo wa kuzalisha vifaa hivyo tunao. Sasa katika mita hizi za umeme pia tunafanya ukaguzi ili kujiridhisha na uwezo wetu," aliongeza Dkt Kalemani.
Alisema kuwa, uzalishaji wa vifaa vya umeme nchini una faida mbalimbali ikiwemo kupungua kwa gharama za usafirishaji, mita kupatikana kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa wingi.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kulia) akizungumza na watendaji wa Kiwanda cha Baobab Energy Systems kinachozalisha mita za umeme nchini . Katikati ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Hashim Ibrahim.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza mara baada ya kufika katika kiwanda cha Baobab Energy Systems kinachozalisha mita za umeme nchini. Wengine katika picha ni watendaji wa kiwanda hicho, Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
za umeme katika kiwanda cha Baobab Energy Systems kinachozalisha mita za umeme nchini. Wengine katika picha ni watendaji wa kiwanda hicho, Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Hashim Ibrahim na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...