Na Zainab Nyamka Globu ya Jamii.
STAND United yapunguza spidi ya Simba!Ndio kauli ambayo unaweza kuitumia baada ya vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba kushindwa kufurukuta mbele ya wapiga debe wa Shinyanga Stand United kwa kukubali sare ya goli 3-3 katika mchezo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliopigwa ndani ya dimba la Uwanja wa Taifa ulichukua dakika 6 timu ya Simba kuandika goli la kuongoza kupitia kwa beki wake Asante Kwasi aliyemalizia mpira uliotemwa na mlinda mlango wa Stand United.
Dakika ya 23, Laudit Mavugo anashindilia msumari wa pili na kufanya usomeke 2-0 ila matokeo hayo hayakudumu ambapo katika dakika ya 36 mchezaji wa Stand United Tariq anamalizia krosi kwa kichwa na kumimina mpira wavuni na matokeo kuwa 2-1.
Baada ya dakika 5 ikiwa ni dakika ya 41 ya kipindi cha kwanza Stand United walisawazisha kupitia kwa Lulambo na matokei kuwa 2-2 mpaka mapumziko.Kipindi cha pili,kilianza kwa kasi na kila timu kusoma mchezo wa mwenzake ambapo Simba walitangulia kupata goli la 3 dakika ya 61 kupitia kwa Nicolaus Gyan.
Hata hivyo kasi ya wachezaji wa Stand United na dakika 6 baadaye mchezaji wa Stand United raia wa Burundi Bigiriama aliisawazishia timu yake na matokeo kuwa 3-3 mpaka kipyenga cha mwisho.Baada ya matokeo hayo Simba anaendelea kukaa kileleni kwa alama 46 wakifuatiwa na Yanga wenye alama 40 wakiwa wamecheza michezo 19.
Matokeo ya Simba na Stand United yameonekana kuwafurahisha zaidi mashabiki na wapenzi wa Yanga kwani alama za Simba kukaa kileleni zimezidi kupungua.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...