Na Rhoda Ezekiel Kigoma,
JUMLA ya wanafunzi 346 wa kidato cha kwanza wilayani Kakonko mkoani Kigoma,wameshindwa kuripoti shuleni kutokana na shule walizopangiwa kuwa na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Hali iliyo walazimu viongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na wananchi kujenga vyumba viwili kwa kila shule.
Akitoa takwimu hizo jana katika ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Kakonko ya kutembelea ujenzi wa vyumba hivyo, Ofisa elimu sekondari wilayani humo Clouds Nzabayanga amesema miongoni mwa wanafunzi 1714 waliofaulu kuingia kidato cha kwanza walishindwa kuripoti ni 346.
Amefafanua wanafunzi hao waliopangiwa katika shule ya Kanyonza, Muhange na Gwanumpu.Amesema katika shule ya Kanyonza kuna wanafunzi 78, Muhange 97 na Gwanumpu 171 ambao bado hawajapewa barua zao za kujiunga shuleni hapo hadi hapo shule hizo zitakapo kamilisha ujenzi wa madarasa hayo.
Ameongeza kila shule inatakiwa kujenga madarasa mawili kwa nguvu za wananchi na Serikali kuchangia mabati pamoja na ukarabati wa vyumba hivyo.Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala ,amewapongeza Watendaji wa kijiji pamoja na Wenyeviti wa kijiji kwa juhudi kubwa walizozionesha za kuwashawishi wananchi kujitoa katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Amesema wameonesha namna ambavyo wanataka iliwanafunzi waanze kupata elimu kama wengine, na kumuagiza mkurugenzi kutoa fedha za mabati na ukarabati ili wanafunzi wapewe barua zao na waanze kuripoti shuleni.
Mkuu huyo alisema Serikali inatamani kuona kila mtoto anapata elimu lakini lazima wazazi wajitoe kutatua changamoto zinazo jitokeza kwakuwa Serikali haiwezi kufanya kila kitu na kutatua changamoto zingine na kuwaagiza Wenyeviti kupita kuchangisha fedha na michango mingine kwa wananchi ili watoto wao wapate elimu.
Ameahidi kuchangia bati 30 katika shule ya Kanyonza na bati 20 kwa shule ya Gwanumpu ambazo zimekwisha kamilisha ujenzi wa vyumba hivyo kwa kiasi na kuwataka walimu na wenyeviti kushirikiana kukamilisha madarasa mawili katika shule ya Muhange.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...