Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) iliketi Machi 25, 2018
katika kikao cha kawaida kinachofanyika kila baada ya miezi mitatu kujadili
masuala mbalimbali ya kiutendaji.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni kama yafuatayo:
1. KUZINDULIWA KWA MPANGO MKAKATI (Stategic Plan) WA MIAKA MINNE
Mara baada ya Uongozi huu wa DRFA kuingia madarakani uliazimia kuandaa
mpango mkakati wa miaka minne ambao ulibuniwa ili kuepuka kuendesha chama
bila mipango iliyoainishwa kabla. Mpango huo utakaozinduliwa siku moja kabla ya mkutano mkuu wa DRFA.
2. MAANDALIZI YA MKUTANO MKUU
Mkutano mkuu wa DRFA umepangwa kufanyika kabla ya mwezi wa sita huku
jukumu la kupanga mahali na tarehe maalum likiachwa kwa Sekretarieti ambayo
itatangaza hivi karibuni. Mkutano huu ni wakikatiba na wajumbe wake wametajwa kwenye katiba, kwa
maana viongozi wa wilaya na vingozi wa vyama shiriki.
3. MAANDALIZI YA MAFUNZO YA UTAWALA NA USIMAMIZI WA SOKA
Baada ya kufanikiwa katika kozi ya kwanza ya makocha wa soka la vijana
iliyomalizika mwanzoni mwa mwezi huu, DRFA inaandaa kozi nyingine awamu hii
ikigeukia upande wa uongozi wa klabu na vyama vya soka. Lengo la kozi hii ni kuwaongezea uwezo na utaalam viongozi wa soka mkoani Dar es
Salaam ili kuhakikisha klabu na vyama vya soka vinaongozwa na watu wenye weledi
kwa manufaa ya soka la mkoa huu na taifa kwa ujumla. Hii itafanyika Aprili katika tarehe itakayotangazwa na sekretarieti hivi karibuni.
Kozi hiyo itafuatiwa na nyingine ya waamuzi ambayo ina lengo la kuongeza idadi ya
waamuzi wenye uwezo mkubwa mkoani Dar es Salaam.
4. MWENENDO WA LIGI YA MKOA
Ligi ya mkoa inaendelea vizuri katika hali ya utulivu bila kuwa na malalamiko mengi
toka kwa klabu. Hii imetokana na usimamizi kabambe uliowekwa na DRFA katika
vituo vyote ili kuhakikisha sheria 17 za soka zinafuatwa wakati wote. Ni imani ya DRFA kwamba usimamizi huo utapelekea kupatikana kwa wawakilishi
watatu watakaokwenda kuonyesha ushindani wa kweli kwenye ligi daraja la pili
ngazi ya Taifa. Ligi hiyo yenye makundi matatu inatarajiwa kumalizika Machi 30 huku mechi zake
zikichezwa kila siku katika viwanja vitano tofauti.
5. UGENI TOKA ZANZIBAR
Kuna uhusiano mkubwa uliodumu kwa miaka mingi kati ya DRFA na chama cha
soka mkoa wa Mjini Magharibi ambapo kila mwezi wa nne vyama hivi
hutembeleana kwa zamu kwa ajili ya kujadili na kupeana ushauri wa masuala
mbalimbali yahusuyo maendeleo ya soka. Mwaka huu DRFA itatembelewa na ndugu zetu wa Zanzibar hivyo kamati hiyo
imeandaa utaratibu wa mapokezi ya maafisa wa chama hicho watakaokuja ikiwa ni
pamoja na mchakato mzima wa uwepo wao hapa jijini Dar es Salaam.
6. MAANDALIZI YA LIGI YA MKOA YA VIJANA (U15) IJULIKANAYO KAMA
NDONDO ACADEMY
Baada kuzalisha makocha 25 wa soka la vijana katika kozi iliyomalizika Machi 10,
DRFA iliwaagiza kwenda kuitumia elimu waliyoipata kwa kufundisha vijana kwenye
vituo mbalimbali kukuza soka la vijana (Academy). Michuano ya Ndondo Academy si tu imeandaliwa kwa ajili ya kuibua vipaji vipya,
bali pia ni katika kupata mwendelezo bora wa progaramu ya maendeleo ya soka la
vijana iliyoanza kwa mafunzo ya ukocha. Ligi hii itasimamiwa kwa pamoja
na Kamati ya Soka la Vijana na Kamati ya Mashindano ya DRFA.
7. MAANDALIZI YA LIGI YA MKOA YA WANAWAKE CHINI YA MIAKA 15 (U15)
Kamati ya Utendaji ya DRFA imegundua kwamba idadi ya wasichana walio na
utayari wa kuchezo soka imepungua na kwamba hakuna chanzo maalum cha
kuzalisha wachezaji wapya. Kwa kuliona hilo DRFA imeamua kufungua 'kiwanda' cha nyota wapya wa soka la
wanawake kwa kuanzisha ligi ya vijana, ligi itakayosimamiwa na Chama cha Soka la
Wanawake, Kamati ya Soka la Vijana na Kamati ya Mashindano ya DRFA.
Ahsante
Karim Boimanda
Afisa Habari na Mawasiliano
DRFA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...