Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amewataka wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi kujitathimini yale waliyoazimia kutekeleza kwa mwaka wa Fedha 2017/18 kama yamefikia lengo ili kuweza kusaidia kuboresha utendaji na kutafutia ufumbuzi masuala ambayo yanakwamisha ufanisi wa kazi na kuwezesha mazingira wezeshi kwa wafanyakazi.
Prof. Mbarawa amesema hayo mkoani Morogoro, wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi ambapo pamoja na mambo mengime amesisitiza umuhimu wa baraza hilo katika kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi wenye tija, staha na upendo.
Ni matarajio yangu kuwa kila mjumbe kwa nafasi aliyonayo katika baraza hili atatumia fursa hii kutoa michango ya mawazo ili iweze kuwa mwongozo mzuri wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, ametoa wito kwa wajumbe hao kuhakikisha kuwa Wizara inashiriki kikamilifu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuwajengea watanzania miundombinu bora na imara ili kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda na hivyo kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya kuifanya nchi yetu iwe na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akizungumza na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi (hawapo pichani), wakati wa ufunguzi wa baraza hilo lililofanyika mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga (katikati), akizungumza na wajumbe wa baraza hilo pamoja na wawakilishi kutoka Taasisi zilizo chini ya sekta hiyo katika kikao cha baraza la wafanyakazi, mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Bi. Elizabeth Tagora akiwasilisha rasimu ya bajeti na mpango wa utekelezaji wa sekta hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi, mkoani Morogoro.
Baadhi ya wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) wakifuatilia maelekezo ya mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), wakati wa ufunguzi wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika mkoani Morogoro.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...