KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari imeianzia kambi Tanzania Prisons huku benchi la ufundi likijinasibu limejipanga kuendeleza ubabe dhidi ya maafande hao.

Timu hizo zinatarajia kuumana Jumapili hii katika Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 1.00 usiku, ukiwa ni mchezo wa raundi ya 29 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, amesema kuwa kikosi hicho kimeanza vema maandalizi yake huku akikiri ushindani mkubwa unaoonyeshwa na wachezaji mazoezini.

“Kila mtu anaonyesha ari ya kutaka kucheza kwa hiyo tutarajie tutakuwa na mechi ya ushindani na mechi ya burudani vilevile,” alisema.

Akizungumzia utofauti wa mchezo huo ukilinganisha na ule wa kwanza waliocheza Uwanja wa Sokoine na kuichapa Prisons mabao 2-0, Cheche alidai kuwa; “Mchezo wa kwanza ushapita na huo unaokuja ni mwingine tofauti na ule wa mwanzo.

“Kwa hiyo tunajipanga tofauti na vile tulivyojipanga mwanzo kwa sababu mwanzoni tulicheza uwanja tofauti na tulikuwa na baadhi ya wachezaji ambao sasa hivi hawapo, lakini sasa hivi tunajipanga kivingine kuhakikisha tunaendeleza ubabe wetu.”

Mabao ya Azam FC kwenye mchezo huo wa ugenini, yalifungwa na washambuliaji Yahya Zayd na Paul Peter.

Alisema kuwa kwa sasa haifikirii mechi ya mwisho dhidi Yanga, anachoangalia ni mchezo ujao dhidi ya Prisons kuhakikisha wanaendeleza ubabe kabla ya kujipanga tena kukipiga na Wanajangwani hao.

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, wataingia kwenye mchezo huo wakitoka kuifunga Majimaji 2-0, matokeo yaliyoifanya kuzidi kujikita katika nafasi ya pili kwa pointi 52, ikiizidi Yanga kwa pointi nne ambayo ina mechi mbili mkononi huku tayari Simba ikiwa imeshatangaza ubingwa na pointi zake 68.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...