Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Al-Najem amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa  Ijumaa 25 Mei 2018, yaliyojikita juu ya namna ya kuimarisha uhusiano kati ya Kuwait na wilaya hiyo kwa sifa ya kipekee, na baina ya Tanzania na Kuwait kiujumla. 

Katika mazungumzo hayo, Balozi Al-Najem alisema kuwa ubalozi uko tayari kushirikiana na Uongozi wa Kigamboni katika kusaidia nyanja mbalimbali husasan afya na elimu, aidha alifungua milango ya kuwasaidia watu wenye ulemavu katika wilaya ya Kigamboni kwa kuwapatia vifaa. Yafaa kueleza kuwa ubalozi wa Kuwait ushawahi kuchimba visima vya maji safi na salama huko Kigamboni vinavyotumiwa na wanafunzi wa shule na wakaazi wanaoishi karibu na shule hizo.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ameishukuru Kuwait kwa misaada inayoitoa kwa Tanzania akitoa mifano msaada wa hivi karibuni kwa Taasisi ya Mifupa ya MOI Dar es Salaam na Hospital ya Benjamin Mkapa Dodoma.
Kando ya mazungumzo, Balozi Al-Najem alimkabidhi Mkuu wa Wilaya vikapu vyenye vyakula vya futari vitakavyogaiwa kwa baadhi ya wakaazi wa Kigamboni wenye mahitaji ambapo Al-Najem alisema vyakula hivyo ni zawadi kutoka kwa raia wa Kuwait kwenda kwa ndugu zao na marafiki zao wa Tanzania, zawadi ambayo ni kutoka Chombo cha Baytu Zakat, Wakfu na Mali ya Amana cha Kuwait.


Baada ya mazungumzo hayo, Mkuu wa Wilaya Hashim Mgandilwa aliongozana na mgeni wake Al-Najem katika ziara ya kukagua Hospitali Kuu ya Wilaya na Kituo cha Afya cha Kigamboni kinachodumia takriban watu 36982 ambapo walitembelea wodi mbalimbali na kusikiliza matatizo na changamoto zinazokabili hospitali na kituo hicho.
Wakiwa katika hospitali ya Wilaya, Balozi Al-Najem aliahidi kusaidia wodi ya wazazi na chumba cha watoto njiti kwa kutoa vifaa vya kisasa vitakavyochangia utoaji wa huduma bora kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga ikiwa ni kuitikia wito wa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt John Magufuli wa kuimarisha huduma za afya nchini.

Kabla ya kuondoka Kigamboni, balozi Al-Najem na mwenyeji wake Hashim Mgandilwa walijumuika na wakaazi wa Kigamboni kusali sala ya Ijumaa katika moja ya misikiti ambapo mara baada ya Sala, Mhe. Balozi aliahidi kurudi tena msikitini hapo kwa kuandaa futari.

Balozi wa Kuwait nchini Mheshimiwa Jasem Al-Najem (kushoto) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa wakimkabidhi mmoja wa wakazi wa Kigamboni, kikapu cha chakula kwa ajili ya ftari.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...