Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali,
Dkt. Hassan Abbasi amewataka waandishiwa habari nchini kutumia
taaluma ya habari kuielemisha jamii juu ya usalama barabarini ili
kupunguza ajali ambazo zimeendelea kusababisha vifo visivyo vya lazima
na ulemavu wa maisha.
Dkt. Abbasi ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua
mafunzo maalumu ya miezi sita juu ya uandishi bora wa habari
zinazohusu usalama barabarani, kwa waandishi wa habari 17 kutoka
vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Ameeleza kuwa ajali za barabarani zitapungua kwa kiwango kikubwa
endapo waandishi wa habari watatumia taaluma yao kuielemisha jamii
juu ya usalama barababrani, kupaza sauti za wananchi pale palipo na
changamoto zinazohitaji usimamizi wa Serikali na pia kuwa sehemu ya
mageuzi yanayofanywa na Serikali kuwaondolea wananchi changamoto za
ajali.
“Zaidi ya watu milioni moja na laki mbili hufariki kila mwaka duniani
kutokana na ajali za barabarani na kati ya vifo hivyo asilimia 90 hutokea
katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Wengi wanaofariki kwa ajali
ni watu wenye umri wa kati ya miaka 15-29 na hivyo kuwa na atahari
kubwa kiuchumi na kijamii,” alieleza Dkt. Abbasi.
Amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia kwa umakini mafunzo
watakayopata ili watumie maarifa watakayoyapata kuleta mabadiliko
chanya kwa jamii na wadau wa usalama barabarani.
Nae Mkurugenzi wa Uhakiki na Ubora kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mohamed Mohamed, amesema
kuwa Wizara pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) wameona ni
muhimu waandishi wa habari kuwa na ufahamu wa kutosha juu ya
masuala ya usalama barabarani kwa kuwa wao wana nafasi kubwa ya
kufikisha elimu hiyo kwa jamii kubwa zaidi.
Dkt. Mohamed ameeleza kuwa watu wengi wamekuwa wakipoteza maisha
katika ajali kutokana na sababu nyingi ikiwemo majeruhi kukosa huduma
za haraka pindi ajali inapotokea kutokana na hospitali kuwa mbali.
Amesema kuwa ili kukabiliana na changamoto ya majeruhi kukosa huduma
za haraka wakati wa ajali, Wizara ipo katika hatua za mwisho kuweka
vituo vya kutolea huduma za dharua (Emergency Medicine Services
Centre) katika barabarani kuu ziendazo mikoani ambapo vitarahisisha
kuwapatia huduma za haraka majeruhi wa ajali.
Waandishi wanaoshiriki mafunzo haya ni pamoja na Abadallah Msuya
kutoka Daily News, Evance Ng’ingo na Adam Ruta kutoka Habarileo,
Agness Mbapu kutoka TBC, Beaty Tesha kutoka TBC Taifa, Aisia
Rweyemamu na Chrispin Gerald kutoka The Guardian, Dickson Kanyika
kutoka Star Tv na Radio Free Africa, Herrieth Makweta kutoka Mwananchi
na Jasmin Shamweku kutoka Redio ABM ya Dodoma.
Waandishi wengine ni Juhudi Felix kutoka FADECO Wilayani Karagwe,
Margaret Malisa kutoka Nipashe, Renatus Mutabuzi kutoka ITV, Sylvanus
Kayela kutoma Mlimani TV, Veronica Mrema kutoka Mtanzania na Vumilia
Kondo kutoka Abood Media ya Morogoro.
Mafunzo haya usalama barabarani kwa waandishi wa habari ni ya tangu
tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016 kwa ushirikiano kati ya Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Shirika la Afya
Duniani.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akiongea wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo maalum kuhusu uandishi wa habari za usalama barabarani jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali akimkabidhi vitendea kazi mwandishi wa Gazeti la Habarileo, Evance Ng’ingo ambaye anashiriki mafunzo maalum ya miezi sita kuhusu usalama barabarani.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...