
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ameshukuru Ushirikiano kati ya Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart ya Israel na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kuokoa maisha ya watu wengi nchini, hususan watoto.
Waziri Mahiga alitoa shukrani hizo leo alipoitembelea taasisi hiyo jijini Tel Aviv, Israel akiwa anaendelea na ziara yake ya siku tatu aliyoianza jana. "Zamani nilijua kuwa mtu akizaliwa na maradhi ya kurithi, mtu huyo hawezi kuishi lazima atakufa, lakini uwepo wa taasisi yenu kumenifanya niondoe itikadi hiyo" Dkt. Mahiga alisema.
Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart imeisifu Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuwa ni moja ya Taasi bora kusini mwa Jangwa la Sahara na kwamba ina uwezo na wataalam wa kufanya upasuaji bila ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi. "Serikali inachotakiwa kufanya ni kuiboresha taasisi hiyo kwa kujenga majengo mapya na kuipatia vifaa zaidi na itakapofanya hivyo itaokoa maisha ya watu na fedha nyingi ambazo zingelitumika kugharamia matibabu nje ya nchi". Mkurugenzi wa taasisi hiyo alishauri.
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo alimweleza Dkt. Mahiga kuwa taasisi ilianzishwa miaka ya 90 kwa madhumuni ya kuokoa maisha ya watoto wenye maradhi ya moyo duniani kote, hususan katika nchi zinazoendelea. Hadi sasa imeshatoa matibabu kwa zaidi ya watoto 460,000 wenye maradhi ya moyo kutoka Afrika, Amerika, Asia na kwingineko.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akiongea na wawakilishi wa Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart ya Israel mara baada ya kuwasili katika taasisi hiyo kujionea namna inavyoendesha shughuli zao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe, Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akimjulia hali mmoja wa watoto kutoka Tanzania anayepata tiba ya maradhi ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Save the Children Heart ya Israel
Kutoka kulia, mtu wa kwanza na wa pili ni Watanzania wanaosomea fani za tiba za maradhi ya moyo katika taasisi ya Save the Children Haert wakiongea na Mhe. Waziri wakati alipoitembelea taasisi hiyo jijini Tel Aviv, Israel leo.
Wanne kutoka kushoto ni wanafunzi kutoka Tanzania wanaosomea fani ya tiba ya maradhi ya Moyo wakimsikiliza Mkurugenzi wao hayupo pichani.
Kaimu Mkurugenzi wa Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Suleiman Salehe akibadilishana mawasiliano na wanafunzi wanaosomea fani ya tiba ya maradhi ya moyo kutoka Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...