Na Greyson Mwase, Tanga

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameipa siku saba kampuni inayojishughulisha na utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wilayani Handeni ya CANACO Tanzania Limited, kuwasilisha mikataba na nyaraka zote kati yake na kampuni ya Tanzania Gold Field Limited ili kubaini namna makubaliano ya mkataba yalivyofanyika ikiwa ni pamoja na ulipaji kodi serikalini,

Biteko aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyasa kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga mara baada ya kufanya ziara katika kampuni ya CANACO Tanzania Limited na kutoridhishwa na utendaji wa kampuni hiyo.

Waziri Biteko yupo katika ziara ya siku mbili mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua shughuli za madini pamoja na kuzungumza na wananchi na kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika shughuli za madini.

Alisema mara baada ya kufanya ziara katika kampuni ya CANACO Tanzania Limited, amebaini kuwa kampuni hiyo mara baada ya kukamilisha shughuli zake za utafiti wa madini ya dhahabu, kampuni hiyo iliikaribisha kampuni nyingine ijulikanayo kama Tanzania Gold Field Limited ya Canada kwa ajili ya kufanya shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo la Magambasi wilayani Handeni mkoani Tanga pasipo kufuata taratibu za kisheria.

Aliendelea kusema kuwa, kampuni ya Tanzania Gold Field Limited iliwataka wachimbaji wadogo waliokuwa wanaendelea na shughuli za uchimbaji madini katika eneo hilo kuondoka ili waanze uchimbaji madini jambo ambalo lilitekelezwa.Alieleza kuwa, kampuni ya Tanzania Gold Field Limited ilianza shughuli zake bila kuwasilisha makubaliano ya kimaandishi kati yake na kampuni ya CANACO Tanzania Limited Serikalini pamoja na kodi jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.

Biteko aliendelea kusema kuwa kampuni inayotambulika mpaka sasa kisheria ni ya CANACO Tanzania Limited ambapo shughuli za madini katika eneo la Magambasi zimekuwa zikifanyika bila kufuata sheria na kanuni za mazingira.

“Haiwezekani wachimbaji wadogo ambao ndio wamiliki wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wakaondolewa halafu akapewa mwekezaji mkubwa ambaye mpaka sasa hakuna kilichofanyika zaidi ya kuchejua mabaki wa udongo wenye dhahabu na kuuza na kuharibu mazingira huku wachimbaji wadogo wenye uwezo wa kuchimba dhahabu wakihangaika na kuishi katika lindi la umaskini,” alisema Biteko.
 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati mbele) akiendelea na ziara katika  eneo la kampuni inayojishughulisha na utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wilayani Handeni ya CANACO Tanzania Limited.

 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ( wa pili kutoka kulia) akitoa maelekezo kwa uongozi wa kampuni  inayojishughulisha na utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wilayani Handeni ya CANACO Tanzania Limited.
 Sehemu wa wananchi wa kijiji cha Nyasa kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akifafanua jambo mbele ya wananchi wa kijiji cha Nyasa kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga (hawapo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe (kushoto) akielezea mchango wa sekta ya madini kwenye wilaya yake mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...