Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo(aliyeinama) wakati alipotembelea maduka ya bidhaa ya mafuta ya kupikia na sukari ,Loliondo ,Mailmoja ,Mjini Kibaha,(Wa pili kutoka kulia) ni kamanda wa polisi wa mkoa huo , (ACP) Jonathan Shanna na wa kwanza kushoto mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoani Pwani ,Abdallah Ndauka.(picha na Mwamvua Mwinyi).

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

SERIKALI mkoani Pwani, imewahakikishia wananchi kuwa inawasimamia wafanyabiashara wa mafuta ya kupikia, washushe bei ya bidhaa hiyo ambayo kwasasa inauzwa lita moja sh. 5,000 kutoka sh. 3,200 iliyokuwa ikiuzwa kipindi cha nyuma.

Aidha imetoa onyo kwa wafanyabiashara wa sukari na mafuta hayo, ambao watajaribu kuficha bidhaa hizo kwa lengo la kujitajirisha haraka haraka baadae kwa kupandisha bei na kudai atakaefanya hivyo atakiona.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo aliyasema hayo wakati alipotembelea maduka ya bidhaa hizo, Loliondo, Mailmoja, Mjini Kibaha huku akiwa ameambatana na kamanda wa polisi wa mkoa huo, (ACP) Jonathan Shanna .
Alisema Mei 16 mwaka huu, waliamua kutembelea baadhi ya magodauni na maduka ya bidhaa hizo ambapo wamejiridhisha kwa kukuta sukari ikiuzwa bei nzuri na maeneo mengine wakishusha madumu ya mafuta kwa ajili ya kuuzia walaji. Ndikilo alieleza kwamba ,hategemei kuona wala kusikia kuna mfanyabiashara atakaefanya kitendo hicho ili bidhaa hizo ziwe adimu .

“Kama yupo mfanyabishara atakaejaribu kuficha mafuta na sukari kwa uroho wa fedha ,atakumbana na mkono wa sheria na hatutosita kumchukulia hatua za kisheria”

“Serikali inachunguza wote watakaoficha bidhaa hizo ,na jeshi la polisi mkoani hapa chini ya kamanda Shanna linaendelea na misako mbalimbali na kusimamia suala hili na wamejipanga”alisisitiza Ndikilo.

Akizungumzia sukari, Ndikilo ambae pia ni mkuu wa mkoa huo,alisema bidhaa hiyo ilikuwa ikiuzwa 2,600 kwa kilo lakini imeshuka hadi 2,400/2,300.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoani Pwani, Abdallah Ndauka aliwataka wafanyabiashara watoe huduma kama inavyostahili na kwa wakati. Aliwaomba wazalishaji wa bidhaa  viwanda kuzalisha na kusambaza kwa wingi bila kuwakwaza wananchi. Ndauka alisema kuwa,kama chama watawashughulikia wafanyabiashara watakaokwamisha jambo hilo na kuwaasa wawe sehemu ya kutoa huduma stahiki hasa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Nae kamanda wa polisi mkoa wa Pwani ,Shanna alisema wameyabeba maagizo yaliyotolewa na kusema wanajua magodauni,store na maduka yote yanayouza bidhaa hizo hivyo asithubutu mfanyabiashara kulijaribu jeshi hilo. Shanna alielezea,ameshayapokea maelekezo kazi yake kubwa ni utekelezaji wa vitendo kwani wanaintelijensia ya kutosha.

Kwa upande wao wafanyabiashara akiwemo Kassim Haji ,alisema mafuta ya kupikia yalipotea lakini kwasasa kuanzia Mei 16 yameanza kuingia na kwa yeye anatarajia kupokea madumu 600. Alisema wanatarajia kushusha bei baada ya kuanza kupelekewa mafuta kwani awali kulikuwa na shida bandarini na anaahidi kushusha gharama ya bidhaa hiyo.

Nao baadhi ya wananchi waliokuwepo soko la Loliondo kwa ajili ya kujinunulia vyakula na bidhaa mbalimbali akiwemo Zulfa Rashid ,alisema bidhaa inayowaumiza ni mafuta ya kupikia. Aliomba mafuta hayo yashushwe bei kwani yanauzwa kwa sh,5,000 kwa lita moja fedha ambayo ni kubwa na maisha ni magumu hasa kuelekea kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Tunaomba gharama zishushwe ,serikali isimamie suala hilo,na tunashukuru mkuu wa mkoa kuja kuzungumza na sisi ,pamoja na kutuhakikishia bidhaa hizo zitashushwa bei.

Zulfa alisema, wengi wao wanatumia nazi na kuacha kununua mafuta kutokana na gharama kupanda tofauti na zamani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...