Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii
MAHAKAMA ya Mkazi Kisutu imeelezwa mkataba uliongiwa na Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando na Channel 2 Group Corporation (BV1) haukujulikana na bodi ya Wakurugenzi wala bodi ya zabuni za TBC.
Mwanasheria wa shirika hilo, Gwakisa Mlawa ameeleza hayo leo Mei mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi alipokuka akitoa ushahidi wake katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh.milioni 887. inayomkabili Tido.
Akiongozwa na Wakili wa Takukuru, Leonard Swai, Gwakisa ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo amedai alifahamu kuwepo kwa mkataba huo baada ya kupelekewa taarifa ya kesi Juni mwaka 2012 na Channel 2 Group Corporation (BV1) ambapo walikuwa wakidai TBC wamekiuka mkataba walioingia kwa ajili ya kuwekeza kwenye mitambo ya digital.
Shahidi huyo alidai, mkataba huo ulisainiwa na Tido na watu wawili wa Channel 2 Group Corporation (BV1) na kwamba kulikuwepo na nyongeza ya mkataba ama marekebisho ya mkataba yaliyosainiwa Juni, Agosti na Novemba mwaka 2008.
Alidai baada ya kupokea taarifa hiyo, TBC ilimwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuomba ushauri na baada ya AG kuliangalia suala hilo Kwa ujumla wake aliagiza ateuliwe mwanasheria wa kimataifa ambaye ni mjuzi katika masuala hayo.
Amedai iliteuliwa kampuni ya uwakili ya Freshfield Bruckhaus Derringer us LLP ambaye baada ya kuteuliwa alifika, TBC na kufanya uchunguzi wa nyaraka na kwamba ililipwa maalipo ya awali zaidi ya milioni 800.
Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa kuwa Tido alisababisha hasara kutokana na kiasi hicho cha fedha hicho ambacho kililipwa kwa kampuni hiyo ya uwakili.
Akijibu swali la Wakili wa Tido, Ramadhan Maleta, kama aliwahi kuiona hiyo mikataba iliyoingiwa na Tido na kwamba ilikuwa ikimpa kazi, channel 2 Group Corporation (BV1) alidai kuwa ilikuwa ni kama wameingia katika makubaliano ya awali ya maandalizi ya mchakato wa kuelekea kwenye digital.
"Wewe kama mwanasheria wa TBC kwa jinsi ulivyoipitia hiyo mikataba ulichukua hatua gani." Aliuliza Maleta,
Akijibu swali hilo shahidi huyo alidai, taarifa ya kesi ilifika wakati akiwa nje ya TBC lakini baadae alirudi. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kesho
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Juni 16, mwaka 2008, akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido aliyekuwa Mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...