Na Veronica Kazimoto,Zanzibar 

Wastani wa ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha miezi 10 ya Mwaka wa Fedha 2017/18 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umeongezeka hadi kufikia asilimia 16 ukilinganisha na asilimia 14 katika kipindi kama hicho cha 2016/17. 

Hayo yamesemwa na Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere baada ya kumaliza Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya hiyo kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambacho TRA ilikuwa mwenyeji.

"Katika kikao hiki tulichomaliza leo, tumejadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafanikio tuliyoyapata ambayo ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato katika Jumuiya yetu kutoka asilimia 14 kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/17 hadi kufikia asilimia16 katika kipindi kama hicho cha Mwaka huu wa Fedha wa 2017/18", alisema Kichere. 

Kichere alieleza kuwa, pamoja na mafanikio hayo, kikao hicho kimejadili na kukubaliana masuala mbalimbali yakiwemo kuimarisha utozaji kodi kwa watu binafsi na wafanyabiashara wadogo na kuweka mipango mahususi ya kutoza kodi stahiki kutoka kwa wafanyabiashara hao. 

"Pia, tumekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kupeana taarifa na kuonyeshana mianya ya ukwepaji kodi ili kudhibiti na kukomesha hali hiyo," alibainisha Kichere.

Makubaliano mengine ni pamoja na kuweka mikakati mahususi ya kushughulikia masuala ya uadilifu kwa kuwa, Mamlaka za Mapato za Afrika Mashariki kama ilivyo kwenye taasisi nyingine za Serikali ndani ya Jumuiya, kumekuwa na changamoto hiyo ya uadilifu. Hivyo, Makamishna Wakuu hao wamekubaliana kuongeza ufanisi katika kukagua mwenendo wa maisha wa watumishi wa Mamlaka zao ikiwa ni pamoja na kuwashitaki wale wote ambao si waadilifu kama sehemu ya kupambana na rushwa. 

"Ndugu waandishi wa habari, pamoja na kupambana na rushwa, tumekubaliana pia kupunguza gharama za mifumo ya TEHAMA kwa kuwajengea uwezo watumishi wa ndani ya Mamlaka ili kupunguza gharama ambazo zinatumika kuwalipa watalaam kutoka katika mataifa mengine," aliongeza Kichere.


Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (katikati) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambapo TRA ilikuwa mwenyeji. Kushoto ni Mhe. Audace Niyonzima wa Mamlaka ya Mapato Burundi na kulia ni Bi. Doris Akol, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA).

 Mwenyekiti wa Kamati ya Watalaam wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mahariki Bi. Martine Nibasumba kutoka Mamlaka ya Mapato Burundi (OBR) akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo kwa Makamishna Wakuu (hawapo pichani) wakati wa Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya hiyo kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambapo TRA ilikuwa mwenyeji.


Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna Wakuu wenzake na baadhi ya wajumbe wa Kikao cha 44 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 29 hadi 30 Mei, 2018 katika Ukumbi wa Benki Kuu, Zanzibar ambapo TRA ilikuwa mwenyeji.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...