Na: Calvin Edward Gwabara-Njombe.

Wakulima Mkoani Njombe wamewashukuru watafiti na Serikali kwa kuwezesha kupatikana kwa mbegu bora za muhogo ambazo zinauwezo wa kustawi kwenye maeneo ya baridi hasa nyanda za juu kusini baada ya utafiti wa mwaka mmoja ulifanywa na watafiti kutoka kituo cha utafiti wa kilimo cha Mikocheni MARI na chuo kikuu cha Dar es salaam.

Wakiongea kwa furaha wakati wa zoezi la kuvuna mihogo hiyo ambayo ilipandwa mwaka mmoja uliopita wakulima hao wamesema sasa wamepata zao la biashara la uhakika baada ya zao la la chai kusumbua biashara yake .

Akiongea kwa niaba ya wakulima wenzake bwana Mapambano Luhongori Mkazi wa kijiji cha Lupembe wilaya ya njombe mkoani humo amesema kuwa Zao la Muhogo sasa litakuwa mkombozi kwa wakulima wengi ambao wamekuwa na shauku ya kulima zao hilo ili kuweza kunufaika na fursa kubwa ambazo wanazipata wakulima wa mikoa mingine kama vile Mara, Geita na Pwani.

‘’ Kutokana na uhitaji na soko kubwa la muhogo mkoani njombe nimejaribu mara kadhaa kulima zao la muhogo bila mafanikio lakini siamini macho yangu leo kuona katika eneo hilihili ambalo tulipanda mbegu hizi bora za watafiti kwenye shamba darasa imetoka mihogo mingi na mizuri kiasi hiki, ila nimegundua kuwa mbegu tulizokuwa tunatumia za kienyeji hazifai ukanda wetu’’ Alisema Luhongoli mkulima kutoka mkoa huo.
Wakulima na wakazi wa kata ya Lupembe Mkoani Njombe wakifurahia mavuno makubwa ya mbegu za Muhogo zinazostawi kwenye maeneo ya baridi kali.
Mtafiti kiongozi wa Utafiti huo Dkt. Joseph Ndunguru akifafanua jambo kwa wakulima mara baada ya kuvuna baadhi ya mashina hayo kwenye kila aina 75 walizopanda eneo hilo. 

Kwa upande wake Bi Rehema Malekela ambaye pia alishiriki kuanzia mwazo wa utafiti mpaka wakati huu wa kuvuna amesema kilimo cha zao hilo kilikuwa kidogo sana ambapo familia zimekuwa zikilima mashina machache kuzunguka nyumba kwaajili ya vitafunywa vya chai tu baada ya kuona zao hilo haliwezi kuwapatia tija kama wakulima wa maene mengine nchini.

Bi Malekela ameongeza kuwa wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani waislamu hupata shida sana kupata muhogo na hivyo kuwalazimu baadahi ya wafanyabiashara wengi kwenda kufuata mihogo kwenye mikoa mingine inayozalisha zao hilo kwa wingi na kuja kuiuza mkoani humo kwa bei kubwa.

“ Kwakweli ukifunua moyo wangu na moyo wa kila mtu unayemuona hapa aliyekuja kushiriki zoezi hili utaona furaha isiyo na kifani ndio maana unaona tumejitokeza kwa wingi watu kutoka Tarafa nzima kuja kushuhudia kupatikana kwa zao linguine la biashara kwenye eneo letu” Alisema Bi. Malekela kwa niaba ya wakina mama wengine.
Mamia ya wakulima na wakazi wa Kata ya Lupembe na maeneo mengine waliojitokeza kuangalia matokeo hayo ya utafiti kuona kama wanaweza kulima Muhogo kwenye ukanda huo wa baridi kali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...