Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 04 Juni, 2018 amezindua Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme, Phase Two – ASDP II).Mpango huo wa miaka mitano utatekelezwa hadi mwaka 2023 kwa gharama ya Shilingi Trilioni 13.8 ambapo Serikali na washirika wa maendeleo watatoa asilimia 40 ya fedha hizo, na sekta binafsi itatoa asilimia 60.
Uzinduzi wa mpango huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda, Mawaziri, Wabunge, Mabalozi, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, wadau wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, wadau wa sekta binafsi, viongozi wa dini na viongozi wa siasa.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi na wataalamu wa Serikali pamoja wadau wengine ikiwemo sekta binafsi, kusimamia vizuri utekelezaji wa mpango huo ambao lengo lake kuu ni kuleta mageuzi katika sekta ndogo za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija, kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi badala ya kujikimu pekee, kuongeza mapato ya wakulima, uhakika wa usalama wa chakula na lishe na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa ujumla.
Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wakulima, wafugaji na wavuvi kuwa Serikali itashirikiana nao kwa karibu katika utekelezaji wa mpango huu, lakini ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji wa benki ya maendeleo ya kilimo ambayo amesema licha ya kuwezeshwa na Serikali mtaji wa takribani Shilingi Bilioni 300 kwa ajili ya kuwakopesha wakulima, imekuwa haiwakopeshi wakulima.
“Naomba niwe mkweli, bado sijaridhika na utendaji kazi wa benki hii, benki ipo pale kwa ajili ya kuwakopesha wakulima, Serikali inakopa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kuwakopesha wakulima, lakini yenyewe inachukua hizo hela na kwenda kuzikopesha benki zingine.
“Kwa hiyo tumekopa pesa kutoka AfDB Shilingi Bilioni 207, mtaji umewekwa na Serikali Shilingi Bilioni 60 tangu mwaka 2014, lakini hakuna fedha iliyokwenda kwa mkulima, na wakati mwingine benki hii inapotaka kukopesha huwatafuta matajiri wakubwa ambao baadhi yao wameshindwa kulipa mikopo yao kwenye benki zingine, sasa nikisema siridhiki na utendaji wa benki hii mtanikatalia ndugu zangu?” amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais amewataka viongozi wa Serikali kutoa taarifa juu ya juhudi za Serikali kuimarisha sekta ya kilimo ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Ukanda wa Kusini (SAGCOT) ambao mwaka 2016 ulipatiwa Shilingi Bilioni 150 za mkopo kutoka Benki ya Dunia na mradi wa kuunganisha matrekta uliopatiwa mkopo wa takribani Shilingi Bilioni 248.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt. Charles Tizeba kuchukua hatua dhidi ya mzigo wa tozo zinatozwa na bodi mbalimbali za mazao nchini, ambazo zimekuwa zikiwaumiza wakulima ilihali bodi hizo hazichangii katika gharama za uzalishaji wa mazao.
Kabla ya hotuba ya Mhe. Rais Magufuli, Mhe. Waziri Tizeba ameeleza kuwa katika utekelezaji wa mpango wa ASDP II Serikali imetenga Shilingi Bilioni 943 kupitia wizara mbalimbali katika bajeti ijayo na washirika wa maendeleo wameahidi kutoa Shilingi Trilioni 1 na Bilioni 900 na kwamba tofauti na awamu ya kwanza ya mpango huu, awamu hii ya pili itajielekeza katika mazao machache ya kipaumbele katika kilimo, mifugo na uvuvi yenye kugusa watu wengi na yaliyochaguliwa kwa kuzingatia mnyororo wa thamani na ikolojia ya kanda za kilomo.
Mhe. Dkt. Tizeba amebainisha kuwa ASDP II inatekelezwa wakati kukiwa na maendeleo mazuri katika sekta ya kilimo ikiwemo kutosheleza mahitaji ya chakula kwa asilimia 123, kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara kutoka tani 796,502 mwaka 2015/16 hadi tani 881,583 mwaka 2016/17 huku kukiwa na uzalishaji mkubwa wa zao la pamba msimu uliopita ambapo umeongezeka kutoka tani 133,000 hadi kufikia tani 600,000.
Nao wawakilishi kutoka kwa wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, Kamati ya Kudumu ya Bunge na washirika wa maendeleo ya sekta ya kilimo wamemuahidi Mhe. Rais Magufuli kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa ASDP II ili malengo yaliyokusudiwa yafanikiwe.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Juni, 2018 .
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP ll) katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julis Nyerere jijini Dar es salaam leo Juni 4, 2018. Anayemshikia kitabu hicho ya Programu ni Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji Ali Hassa Mwinyi nakala ya kitabu cha Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP ll) baada ya kuizindua katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julis Nyerere jijini Dar es salaam leo Juni 4, 2018.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan nakala ya kitabu cha Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP ll) baada ya kuizindua katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julis Nyerere jijini Dar es salaam leo Juni 4, 2018.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan nakala ya kitabu cha Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP ll) baada ya kuizindua katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julis Nyerere jijini Dar es salaam leo Juni 4, 2018.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Mahamoud Hassan Mgimwa nakala ya kitabu cha Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP ll) baada ya kuizindua katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julis Nyerere jijini Dar es salaam leo Juni 4, 2018.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Profesa Raphael Tihela Chibunda nakala ya kitabu cha Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP ll) baada ya kukabidhiwa katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julis Nyerere jijini Dar es salaam leo Juni 4, 2018.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Mwenyekiti wa Taasisi za Sekta Binafsi (TPSF) Dkt. Reginald mengi nakala ya kitabu cha Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP ll) baada ya kukabidhiwa katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julis Nyerere jijini Dar es salaam leo Juni 4, 2018. Picha na IKULU
HABARI ZAIDI BOFYA HAPA
HABARI ZAIDI BOFYA HAPA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...