Na Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Waweka Hazina na Wahasibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za Umma kupitia mfumo mpya wa malipo (epicor 10.2) unaotarajia kuanza kutumika na mamlaka hizo kuanzia  Julai 1 mwaka huu.
Hayo yameelezwa leo, Jijini Dodoma na Mhasibu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Jeremiah Mtawa alipokuwa akifunga mafunzo ya siku nne ya kuwajengea uwezo wa namna ya kutumia mfumo mpya wa malipo (epicor 10.2) Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha na Manyara.
“Kuanzia Julai 1 mwaka huu mfumo wa epicor 10.2 ndio utakaotumika katika kuonesha mapato na matumizi ya fedha za Umma katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini, hivyo mfumo huu ukatumike kama ulivyopangwa na kwa usahihi,” alisema Mtawa.
Aidha amewataka Wahasibu hao kutumia mfumo huo vizuri kwani umeunganishwa na mfumo unaowezesha mabenki kulipana Tanzania (TISS) ambao utaruhusu malipo yote kufanyika kwa njia ya kielektroniki. Hivyo basi, kama mfumo huo utatumika vibaya basi Mhasibu husika atafunguliwa kesi.
Kwa upande wake, Kaimu Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Bibi Mariamu Nkanyanga ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo amesema epicor 10.2 itasaidia kutekeleza kwa asilimia kubwa shughuli ambazo zimeelekezwa katika bajeti ya mwaka husika kutokana na mfumo huo kutoruhusu malipo nje ya bajeti na ikiwa malipo yoyote yatafanyika  nje ya bajeti basi yataonekana kwenye mfumo huo tofauti na mfumo unaotumika sasa.
Nae, Mhasibu wa Halmashauri ya Mji wa Babati Bw. Ajuaye Jasho amesema mfumo mpya wa malipo (epicor 10.2) utaondoa matumizi holela ya fedha za Umma kutokana na matumizi yote ya Halmashauri kuidhinishwa na Mweka Hazina tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo kuna matumizi yalikuwa yakiidhinishwa na Mweka Hazina na matumizi mengine yalikuwa yakiidhinishwa na Mhasibu yeyote wa Halmashauri husika.
Mafunzo ya mfumo mpya wa malipo (epicor 10.2) yanaendelea kutolewa katika vituo Sita nchini ambavyo ni Dodoma, Mbeya, Iringa, Mwanza, Kagera na Mtwara yakihusisha Waweka Hazina, Wahasibu, Maafisa Manunuzi, Wakaguzi wa Ndani na Maafisa TEHAMA, lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo watumiaji wa mfumo huo namna ya kutumia mfumo huo unaotarajia kuanza kutumika Julai 1 mwaka huu na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini.
 Mhasibu Mwandamizi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Jeremiah Mtawa akiongea na Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha na Manyara (hawapo pichani) kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya mfumo wa epicor 10.2, alipokuwa akifunga mafunzo ya siku Nne ya mfumo huo kwa Waweka Hazina na Wahasibu, leo Jijini Dodoma. Mfumo huo unaotarajia kuanza kutumika Julai 1 mwaka huu na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini.
 Mhasibu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Simeon Mwanjwango  (aliyesimama) ambaye ni mwenyekiti wa darasa la mafunzo ya mfumo wa malipo (epicor 10.2) kwa Waweka Hazina na Wahasibu wa Halmashauri za Mikoa ya Arusha na Manyara akitoa maelekezo kwa mgeni rasmi Bw. Jeremiah Mtawa (hayupo pichani) namna walivyopokea mafunzo ya epicor 10.2, wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo,  leo Jijini Dodoma.
Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha na Manyara wakimsikiliza mgeni rasmi Bw. Jeremiah Mtawa (hayupo pichani) alipokuwa akifunga mafunzo ya siku nne ya kuwajengea uwezo Wahasibu hao namna ya kutumia mfumo mpya wa malipo (epicor 10.2) unaotarajia kuanza kutumika na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini kuanzia Julai 1 mwaka huu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...