Na Mariam Mwayela,Njombe

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kutoa huduma, elimu na kusajili walipakodi wapya katika maeneo ya Ludewa, Matamba, Ilembula, Mlangali, Ikonda na Makete Mkoani Njombe ambapo mpaka sasa jumla ya walipakodi 351 wamesajiliwa.

Zoezi hili limekuwa na muitikio mkubwa kutoka kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa na shauku ya kupatiwa elimu ya kodi na kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).

Akizungumza wakati wa kampeni hiyo Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Bw. Richard Kayombo amewashukuru wakazi wa maeneo hayo kwa kuitikia wito na kuonyesha shauku ya kutaka kujua mambo mbalimbali yanayohusu kodi hususani usajili wa biashara, kuhakiki TIN na kusajili walipakodi wapya.

“Tunashukuru sana kwa muitikio huu ulioonyeshwa katika zoezi hili hapa mkoani Njombe ambao unaonyesha uzalendo wa kuchangia mapato ya Serikali kwa kujisajili na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi ambayo ni mwanzo wa kutimiza wajibu wa kulipa kodi”, Alisema Kayombo.

Kayombo amewaambia wafanyabiashara waliofika katika kampeni hiyo, kuwa na ukaribu na maafisa wa TRA ili kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali katika kila hatua ya ulipaji wa kodi na kutoa maoni yao ambayo yataboresha huduma zitolewazo na Mamlaka.

Aidha, Kayombo aliwakumbusha kulipa kodi sahihi na kwa wakati ili kuepuka faini na adhabu zinazoambatana na ucheleweshaji huo. Vilevile, aliwasisitiza umuhimu wa kutunza kumbukumbu sahihi za biashara, kutoa risiti pindi wanapouza bidhaa au huduma na kudai risiti kila wanapofanya manunuzi mbalimbali.

Naye William Kabupa ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wa duka la Nguo eneo la Ilembula, ameishukuru TRA na kusisitiza kuwa, zoezi hili ni zuri na litasaidia wafanyabiashara kutokuwa na sababu ya kukosa TIN au kukataa kulipa kodi.

“Nimefurahi sana kupata TIN yangu leo hapa Ilembula kwani ilikuwa inanibidi kusafiri kwenda Njombe mjini kupata TIN. Aidha, nashauri wafanyabiashara wenzangu wa Ilembula wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata elimu na kusajiliwa ili waweze kulipa kodi na kujivunia kuwa mmoja wa wachangiaji wa mapato ya Serikali” alisema Kabupa.

Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na kampeni ya kutoa Elimu, Huduma na kusajili walipakodi wapya Mkoani Njombe ambapo hadi sasa Walipakodi wa Wilaya za Makete, Ludewa, Wanging’ombe na Njombe wanaendelea kupata huduma, elimu na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...