WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka asasi zisizokuwa za Serikali (NGOs) zitekeleze majukumu yake kama ambavyo zimesajiliwa na ziache kufanya shughuli zilizo nje ya makubaliano.

Amesema Serikali itaendelea kuzichukulia hatua NGOs zote zinazokiuka taratibu kwa kufanya majukumu mengine kinyume na malengo yake.Ametoa onyo hilo leo (Alhamisi, Juni 7, 2018) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Longido, Dkt. Stephen Lemomo Kiruswa kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

“Serikali itaendelea kuzifuatilia NGOs zote zinazokiuka taratibu na kufanya majukumu mengine yanayozua mitafaruku kwenye jamii na Serikali,” amesema.Dkt. Kiruswa alitaka kufahamu ni lini Serikali itazifutia usajili NGOs zote ambazo kwa muda mrefu zimeacha kutekeleza majukumu yake na badala yake zinafanya shughuli za uchochezi.

Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ina utaratibu wa kufuatilia taasisi hizo kubaini endapo zinafanya kazi kama zilivyojieleza kwenye usajili wake.Amesema mara inapobainika kwamba kuna NGOs ambazo zimeacha majukumu yake na zinafanya shughuli zingine nje ya mikataba yao, hatua stahiki huchukuliwa, hivyo alizitaka zijikite katika utoaji wa huduma bora kwa jamii.

“Kwa hiyo nitoe wito kwa NGO’s zote ambazo Serikali imeridhia na tumezisajili ili ziweze kufanya kazi ya kutoa huduma za jamii, zijikite kutoa huduma za jamii kama ambavyo tumekubaliana, ili tuweze kufikia malengo ya pamoja kati ya Serikali na taasisi zisizo za kiserikali katika kutoa huduma kwa Watanzania wote,” amesema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...