Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii
HAKIMU Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi 9 wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe amegoma kujitoa katika kesi hiyo kwa sababu sababu zilizowasilishwa na washtakiwa hazina mashiko.
Hakimu Mashauri wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ametoa uamuzi huo leo Julai 10 mwaka 2018 na kueleza sababu zote zilizowasilishwa na washtakiwa katika kesi hiyo hazina uhalisia wala mashiko hivyo ombi la kumtaka ajitoe analikataa.
Akichambua hoja saba kati ya hoja zaidi ya kumi zilizowasilishwa na washtakiwa hao ili ajitoe, Hakimu Mashauri amesema kuhusu kuripoti Polisi kila Ijumaa hilo sharti lilitolewa kwa mujibu wa sheria na kama upande wa utetezi hawakuridhika na wanawakilishwa na mawakili wasomi wangeomba rufaa.
Pia alibainisha kuwa hoja zote zilizowasilishwa na washtakiwa hao hazina mashiko ya kutosha na akazikataa miongoni mwao ni pamoja na za Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye alidai kuwa yeye ana Imani naye kwanza, masharti ya dhamana waliyopewa na mahakaama hiyo kuripoti kila siku ya Ijumaa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam katika kipindi cha miezi mitatu mfululizo ni adhabu tosha.
Pia alidai washtakiwa saba kati ya tisa ni wabunge na wanamajukumu makubwa ya kitaifa kama kushiriki katika vikao vya bunge la bajeti, hivyo mheshimiwa hakimu unatambua kuwa kipindi tunaripoti kituo cha polisi , bunge lilikuwa linaendelea na vikao vya bajeti Dodoma na hivyo kulazimika sisi viongozi kwenda Dodoma na kurudi Dar kwa ajili ya kuripoti polisi.
Hakimu Mashauri katika Uamuzi wake amesema, washtakiwa katika kesi hiyo wanatetewa na mawakili, na kama hawakuwa wameridhika na masharti hayo ya dhamana wangeweza kukata rufaa
Washtakiwa katika Kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na mbunge wa bunda, Esther Bulaya.
Wengine ni katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji, mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.
Washtakiwa kwa pamoja wanakabiiwa na mashtaka 13, ambapo katika shtaka la kwanza la kula njama, kwa pamoja Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam walikuĺa njama pamoja na wenzao ambao hawapo mahakamani walikula njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali, mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko kutawanyika
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...