Na Asteria Muhozya, Dodoma

Waziri wa Madini Angellah Kairuki jana tarehe13 Agosti alikutana na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mheshimiwa Thami Mseleku. Katika mkutano huo, Balozi huyo alimueleza Waziri Kairuki kuhusu utayari wa Nchi hiyo ya Afrika Kusini kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta ya madini nchini.

Ujio wa Balozi Thami Mseleku, Makao Makuu ya Wizara ya Madini, unafuatia ziara ya Kamati ya Jamii na Masuala ya usalama ya Bunge ya Jimbo la Gauteng Pretoria- Afrika Kusini ambao walifika nchini mwezi Juni mwaka huu kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa namna sekta ya madini nchini inavyoendeshwa.

Aidha, wakati wa ziara ya kamati hiyo ya Bunge hilo nchini, ilikubalika kuwa na haja ya kuwa na ushirikiano katika masuala mbalimbali ya namna ya kusimamia sekta ya madini ikiwa ni pamoja na shughuli za uchimbaji madini, kubadilishana uzoefu katika udhibiti wa uchimbaji holela wa madini, usimamizi wa migodi na wachimbaji wadogo wa madini.

Maeneo mengine ni pamoja na namna ya kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini kutoka katika uchimbaji mdogo kwenda katika uchimbaji wa kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa.Pia, masuala ya utafiti wa miamba ya uchimbaji madini, mafunzo kwa ajili ya wataalam, kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa sekta ya madini, masuala ya umiliki wa migodi na namna ya kuwawezesha wazawa kumiliki uchumi kupitia sekta ya madini.

Kwa upande wake, Waziri Kairuki alimhakikishia Balozi Thami kuhusu nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kumarisha na kukuza zaidi mahusiano baina ya nchi hizo mbili pamoja na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika sekta mbalimbali hususan katika sekta ya madini ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili.Vilevile, Waziri Kairuki alimueleza Balozi huyo jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ambapo ameendelea kuwakaribisha zaidi wawekezaji kutoka Afrika Kusini kuwekeza katika sekta ya madini nchini.

Vilevile, Waziri Kairuki alimpa pole Balozi huyo kufuatia kifo cha Mama Winnie Mandela aliyefariki dunia mwezi Aprili mwaka huu.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akimweleza jambo Balozi ya Afrika Kusini nchini Tanzania Thami Mseleku (kushoto) wakati Balozi huyo alipomtembelea Waziri kairuki ofisini kwake jijini Dodoma.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania Thami Mseleku, wakijadiliana jambo ofisini kwa Waziri Kairuki, jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...