Serikali imesema haitamwongezea mkataba mkandarasi China Railway 15
Bureau Group Corporation anayejenga barabara ya Chunya –Makongolosi
kwa kiwango cha lami muda wake utakapomalizika.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias John Kwandikwa amesema muda wa
miezi 27 aliyopewa kujenga barabara hiyo yenye urefu wa KM 39
unatosha na hivyo ni jukumu lake kuhakikisha kuwa anakuwa na vifaa na
wafanyakazi wa kutosha wakati wote.
“Mkishindwa kukamilisha barabara hii kwa wakati hamtapata tena kazi
hapa nchini kwani mtakuwa mmeshindwa kazi kwa kukiuka mkataba na
kuiongezea Serikali gharama”, amesema Mhe. Kwandikwa.
Naye Kaimu meneja wa wakala wa barabara (TANROADS) mkoa wa
Mbeya Mhandisi Selemani Lawena amesema barabara ya Chunya
–Makongolosi ni sehemu ya barabara ya Mbeya-Rungwa yenye urefu wa
KM 293 ambayo inaunganisha kwa njia fupi mkoa wa Mbeya na mikoa ya
Singida na Tabora.
“Barabara hii ikikamilika itafungua uchumi wa mikoa ya Mbeya na Songwe
na kuhuisha shughuli za kilimo,mifugo, uchimbaji madini na ufugaji nyuki
na hivyo kuongeza fursa za maendeleo kwa jamii na serikali kwa ujumla”,
amesema mhandisi Lawena.
Mhandisi lawena amesema sehemu ya Mbeya- Chunya KM 72 imekamilika
na ujenzi wa Chunya –Makongolosi KM 39 unatarajiwa kukamilika Januari
2020.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa amekagua ujenzi wa
barabara ya mchepuo ya Iwambi-Mbalizi KM 6.5 jijini Mbeya ambayo
itatumiwa na magari madogo ili kupunguza msongamano na ajali katika
mlima Mbalizi na kusisitiza umuhimu wa wadau wote wa usafiri kushirikiana
ili kupunguza ajali na hivyo kulinda maisha na mali.
Ujenzi wa daraja la Kikamba wilayani Songwe linalounganisha Mkoa wa
Songwe na Katavi ukiendelea daraja hilo linatarajiwa kukamilika mwishoni
mwa mwaka huu.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa akisisitiza jambo kwa
Mbunge wa Songwe Mhe. Philipo Mulugo alipokagua ujenzi wa daraja la
Kikamba wilayani Songwe, daraja hilo linaunganisha Mkoa wa Songwe na
Katavi.
Muonekano wa barabara ya Chunya –Makongolosi KM 39 ambayo ujenzi
wake unaendelea, barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Mbeya-
Rungwa yenye urefu wa KM 293 inayounganisha kwa njia fupi mkoa wa
Mbeya na mikoa ya Singida na Tabora.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Mbeya
mhandisi Selemani Lawena wa kwanza (kulia), akitoa taarifa ya ujenzi wa
barabara ya Chunya –Makongolosi KM 39, kwa Naibu Waziri wa Ujenzi
Mhe. Elias John Kwandikwa (wa tatu kulia), alipokagua ujenzi huo,
(katikati) ni Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mary-Prisca Mahundi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...