Na Benny Mwaipaja, WFM, Mtwara

WAKAZI wa Kijiji cha Kilambo, Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara, wameiomba Serikali iwasaidie kuwatafutia mwekezaji atakayejenga kiwanda cha kusindika matunda na mazao ya kilimo katika kijiji chao kutokana na kijiji hicho kuwa na matunda na mazao mbalimbali yanayokosa soko na kuwasababishia umasikini.

Wakazi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo Bw. Mohamed Mkama, wametoa ombi hilo mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, aliyefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Forodha cha Kilambo, kilichoko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, mkoani Mtwara, kwamba kijiji chao kina fursa nyingi za kilimo zinazohitaji viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yao na kutoa ajira kwa vijana.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo Bw. Mohamed Mkama, alisema kuwa Kijiji chao kinapakana na nchi ya Msumbiji ambako kuna mwingiliano mkubwa wa watu katika masuala ya biashara na uhusiano wa kijamii ikiwemo pande
mbili za nchi kuoleana hivyo kuwafanya wananchi wa Msumbiji waishio mpakani kutegemea bidhaa kwa wingi kutoka katika kijiji chao.

"Watu kutoka Msumbiji wananunua sana chakula na bidhaa nyingine kutoka kwetu lakini tunawauzia bidhaa bila kuongeza thamani hivyo uwepo wa kiwanda utakuza uchumi wa kijiji chetu na tunakuomba Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, utusaidie kupata kiwanda ili nasi tuweze kunufaika" alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Kijiji

Mkazi mwingine wa Kijiji hicho Bw. Selemani Kumamba, alimweleza Waziri wa Fedha na Mipango kwamba Kijiji chao ni maarufu kwa kilimo cha matunda hivyo wanapendekeza kujengwa kwa kiwanda cha kusindika matunda ili juisi itakayozalishwa katika kijiji chao iwe na soko.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kushoto), akitoka kukagua Kituo cha Forodha na Ushuru cha Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA katika Mpaka wa Tanzania na Msumbiji (Kilambo), alipofanya ziara na kuzungumza na wafanyakazi wa Kituo hicho, mkoani Mtwara.
 Meneja wa Kituo cha Forodha na Ushuru cha Kilambo, mpakani mwa Tanzania na Msumbiji mkoani Mtwara Bw. Emmanuel William (wa tatu kulia), akitoa maelezo ya eneo jipya la ujenzi wa Ofisi za Kituo hicho katika Kijiji cha Kilambo, mpakani mwa Tanzania na Msumbiji. 
 Diwani wa Kata ya Tangazo Bw.(kushoto), akijadili jambo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), alipokutana na wakazi wa Kijiji cha Kilambo, akiwa katika ziara yake ya kukagua Kituo cha Forodha na Ushuru-Kilambo, kilichoko mpakani kwa Tanzania na Msumbiji.
 Wazee wa Kijiji cha Kilambo wakimpongeza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) kwa utendaji wake mzuri wa kazi, alipofanya ziara ya kutembelea Kituo cha Forodha katika Mpaka wa Tanzania na Msumbiji- Kilambo Mkoani Mtwara.
 Mzee Seleman Kumamba (kushoto) akizungumza na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), ambapo alimuomba Waziri huyo kuangalia uwezekano wa kuweka kiwanda katika eneo hilo  kikiwemo cha kusindika matunda kwa kuwa watanufaika kutokana na soko la mazao yao lililopo nchi jirani ya Msumbiji.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...