
HAI, KILIMANJARO-
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amekata mzizi wa fitna ambapo ameagiza waliokuwa wafanyakazi wa chama cha ushirika katika eneo la Lambo Estate Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro kutoondolewa katika eneo hilo na kila mmoja kupatiwa ekari mbili kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kimaisha.
Uamuzi huo wa Lukuvi wa kutoa ekari mbili kwa wananchi 78 unafanya kutolewa kwa jumla ya ekari 156 kati ya ekari 1600 na unatokana na mgogoro wa muda mrefu baina ya waliokuwa wafanyakazi wa ushirika na uongozi .Mgogoro uliibuka baada ya wafanyakazi hao kutakiwa kuondoka katika makazi yaliyopo kwenye eneo la shamba kutokana na utumishi wao kukoma.
Waziri Lukuvi alitoa maamuzi hayo katika wilaya Hai ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kutembelea wilaya za Hai, Moshi na Same kushughulikia migogoro ya ardhi katika wilaya hizo mkoa wa Kilimanjaro. Mhe Lukuvi ameshangazwa na ushirika wa watu wachache kutaifisha ardhi na kuamuru watu waliokuwepo muda mrefu katika eneo la lambo estate kuondoka na kusema kuwa safari hii serikali itawanyoosha wale wote wanaofanya ujanja wa kuwaonea wanyonge.
*”Sijawahi kuona ushirika wa namna hii ambapo wenye rasilimali hawanufaiki na ardhi iliyopo katika kijiji chao halafu ardhi hiyo inakodishwa kwa wanachama wa ushirika wanaotoka vijiji vingine”* alisema Waziri Lukuvi.
Huku akishangiliwa na wananchi wakati akitoa maamuzi hayo, Mhe. Lukuvi alisema amekwenda katika eneo hilo la Lambo Estate kushughulikia mgogoro wa ardhi. Suala la ushirika litashughulikiwa na waziri mwenye dhamana na vyama vya ushirika ambae ataamua iwapo ushirika huo unafaa. Waziri Lukuvi alisisitiza kuwa, serikali haiwezi kuwaondoa wazee walioishi kwa muda mrefu.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...