Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC zinatakiwa kukuza uelewa wa shughuli za SADC kwa wananchi wake kwa kufundisha mashuleni historia ya ukombozi wa nchi hizo pamoja na kutumia wimbo wa SADC na bendera yake kwenye shughuli za kitaifa na kimataifa.
Baraza la SADC la Mawaziri wa nchi wanachama wanaoshughulikia sekta za Mawasiliano, Habari, Ujenzi na Uchukuzi walikubaliana hayo katika kikao kilichofanyika Septemba 27,2018 Windhoek, Namibia baada ya kufunguliwa na Waziri wa Madini na Nishati wa Namibia Mheshimiwa Tom Alweendo kwa niaba ya Makamu wa Rais wa nchi hiyo.
Kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC kilisema wananchi wa SADC wanatakiwa kuelimishwa kuhusu SADC kwa kufahamu historia yake na ukombozi wa nchi wanachama, alama za SADC zikiwemo bendera, nembo, wimbo na itifaki yake kwa kuhusisha elimu hiyo kwenye mtaala wa elimu kwa nchi wanachama.
Akifungua kikao hicho, Waziri wa Madini na Nishati wa Namibia Mheshimiwa Alweendo alisema kuna taarifa nyingi nzuri za kuwaeleza wananchi wa nchi wanachama kuhusu SADC hivyo ni jukumu la Serikali za nchi za SADC kuelimisha na kuwaeleza wananchi wake wakati chombo hicho kkiendelea kujiimarisha.
Kikao hicho cha siku moja kilichokutana kwa lengo la kupitia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi wanachama kwenye maeneo ya sekta za Mawasiliano, Habari, Ujenzi na uchukuzi kilisimama kwa dakika moja kabla ya kuanza ili kuonyesha masikitiko yao kwa vifo vya watanzania zaidi ya 200 vilivyotokana na ajali ya MV Nyerere Ziwa Victoria, Mwanza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...