Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akizungumza na waendelezaji wa miradi midogo ya umeme wanaonufaika na ruzuku ya Mfuko wa Nishati Vijijini ulio chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Kikao kimefanyika jijini Dodoma katika ofisi za Wizara ya Nishati.
Na Teresia Mhagama, Dodoma

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuangalia upya gharama za umeme zinazotozwa na wazalishaji binafsi wa umeme kwa wananchi ili kuwa na muongozo wa pamoja badala ya kila mzalishaji  kutoza gharama yake. Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao chake na waendelezaji wa miradi midogo ya umeme wanaonufaika na ruzuku ya Mfuko wa Nishati Vijijini ulio chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

“ Suala la gharama za matumizi ya umeme wanazotozwa wananchi lazima EWURA mpitie upya na kuweka muongozo, mfano kuna wananchi waliopo vijijini wanatozwa shilingi 750 kwa uniti moja badala ya shilingi 100 na unaweza kuta gharama anazotoza  mzalishaji  wa umeme jua wa eneo moja  zinatofautiana na mzalishaji wa umeme jua wa eneo jingine,” amesema Dkt Kalemani.

Amesema kazi ya kujadili bei za umeme ishirikishe pia watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na REA na kueleza kuwa kama kuna sababu za msingi zinazosababisha wazalishaji  hao wa umeme kutofautiana katika utozaji wa bei za umeme, ziwekwe wazi kwa Serikali. Aidha, Dkt Kalemani amewaeleza wazalishaji hao wa umeme kuhusu  msimamo wa Serikali wa kuunganisha umeme vijijini kwa gharama ya shilingi 27,000 tu kwani kuna wananchi wamekuwa wakilalamika kutozwa gharama kubwa.

Dkt Kalemani amewakumbusha kuzingatia gharama hiyo ya Serikali baada ya wazalishaji hao kutaja gharama za uunganishaji umeme wanazotoza katika maeneo tofauti, ambapo sehemu nyingine wananchi wanatozwa shilingi 40,000 au 150,000 au 50,000 na sehemu nyingine wanaunganishwa kwa kukatwa katika bili za umeme.

Katika kikao hicho, wazalishaji hao wameeleza kuhusu utekelezaji  wa kazi ya kuunganishia umeme wananchi ambapo Waziri aliwapongeza kwa kazi hiyo ambayo imepelekea wateja zaidi ya 10,000 kuunganishwa na umeme na vijiji zaidi ya 40 kusambaziwa umeme. Hata hivyo, Dkt Kalemani amewataka kukamilisha kazi ya usambazaji umeme kwa maeneo waliyopangiwa ifikapo Juni 2019, na kuwataka Mameneja wa TANESCO kuhakikisha kuwa wanasimamia pia miradi hiyo badala ya kusimamia miradi ya Serikali pekee ili kuhakikisha kuwa inafanyika kwa ufanisi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na watendaji wa Wizara ya Nishati, REA na TANESCO wakiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasimali Watu, Raphael Nombo ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...