MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti ameagiza wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite (WanaApolo) wapite bila kulipa kwenye lango la kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini hayo hadi hapo utaratibu wa kulipia sh70,000 ili wapatiwe vitambulisho vya kupita utakapofanyika. 

Uamuzi huo umepokelewa kwa mikono miwili na wananchi wa mji mdogo wa Mirerani kwani awali waliokuwa wanaruhusiwa ni wale wenye mkataba wa kulipwa mshahara pekee. 

Mnyeti akizungumza na wadau wa madini alisema wanaApolo watapita bila kulipa chochote kwenye lango hilo hadi hapo vitambulisho maalum vitakapoandaliwa ambavyo watalipia kila mmoja sh70,000 kwa mwaka mmoja. Alisema wamekubaliana kwenye kikao cha wamiliki wa migodi na wanaApolo kuwa suala la malipo ya mishahara au asilimia 10 pindi madini yakitoka wataamua wao wenyewe. 

"Baada ya serikali kukubaliana na pendekezo lenu la kuachana na suala la mishahara ambalo lipo kisheria inabidi ikusanye kodi ya mshahara na tozo ya uendelezaji ufundi stadi," alisema Mnyeti. Mbunge wa jimbo la Simanjiro James Ole Millya alisema wanamshukuru Mnyeti kwa uamuzi huo kwani utawanufaisha watu wengi. 

Aliwataka wamiliki wa migodi na wachimbaji wote kutimiza wajibu wao huku wakitilia mkazo suala la ulipaji wa kodi kwa ajili ya maendeleo.Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, (Marema) Justin Nyari alisema Mnyeti ameweka historia kwa tamko hilo kwani baadhi ya wachimbaji waliondoka ila sasa watarudi. 

Nyari alisema wao kama viongozi wa wachimbaji watakutana na makundi yote yanayojihusisha na madini hayo ili kuweka utaratibu mzuri wa kufanya shughuli hiyo na wanaApolo kutohama hama. Katibu wa Marema tawi la Mirerani, Omary Mandari alisema wanampongeza Rais John Magufuli kwa kujenga ukuta huo na mkuu wa mkoa kwa uamuzi wake wa kuruhusu watu kupita. 

Mandari alisema utaratibu huo wa kuingia bila malipo wakati huu ikisubiriwa vitambulisho maalum ni mzuri tofauti na hapo awali ambapo wanaApolo ilitakiwa waingie kwa kutumia mikataba ya mishahara. Makamu Mwenyekiti wa usalama, afya na mazingira wa shirikisho la wachimbaji madini nchini (Femata) Dk Bernard Joseph alisema wamejipanga kuhakikisha utunzaji mazingira na afya za wafanyakazi. 

Dk Joseph alisema wameweka utaratibu wa wafanyakazi wanaofanya shughuli migodini ikiwemo kuumia, uokoaji na kufukiwa tukishirikiana na wachimbaji wazoefu na Wizara ya Madini. 
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akipokelewa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na polisi kwenye geti la Magufuli la kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro. 
 Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (Marema) Justin Nyari akizungumza kwenye kikao cha wadau wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro. 
 Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ASP Evarest Makala akielezea mikakati ya ulinzi na usalama. 
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Pastory Mnyeti akizungumza kwenye kikao cha wadau wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...