Waziri Ummy Mwalimu akitoa tamko la siku ya ukoma Duniani ambapo aliwasisitiza wananchi kujenga tabia ya kuchunguza miili yao pamoja na watoto kama kuna mabaka rangi ya shaba yasiyo na hisia na kuwahi hospitalini mara waonapo dalili hizo.
========== ========= ============== ==============
TAMKO
LA MHE. UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA
WATOTO KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA UKOMA DUNIANI TAREHE 27/01/2019
KIGAMBONI,
DAR ES SALAAM
Ndugu wanahabari,
Siku ya Ukoma Duniani huadhimishwa ulimwenguni kote kila
Jumapili ya mwisho ya mwezi Januari. Kwa mwaka huu, siku hii
itaadhimishwa tarehe 27 Januari, 2019.
Lengo
kuu la maadhimisho haya ni kukumbusha umma wa watanzania juu ya ugonjwa huu. Ni
dhahiri kuwa ugonjwa wa Ukoma umekuwa ukiogopwa sana katika jamii yetu toka
enzi na enzi hasa kutokana na ukweli kwamba unasababisha ulemavu wa kudumu
mwilini na kufanya waathirika kuwa tegemezi na kutothaminiwa.
Sanjali na madhimisho haya, hapa Tanzania
tunaadhimisha miaka 60 ya uwepo wa Shirika la Ujerumani linaloshughulikia
masuala ya Kifua kikuu na Ukoma (GLRA). Shirika hili limekuwa mstari wa mbele
katika kuisaidia serikali kuhakikisha Ukoma unatokomezwa kwa kufadhili shughuli
mbali mbali ikiwa ni pamoja na kutoa vyombo vya usafiri kwa waratibu wa Kifua
kikuu na Ukoma nchi nzima.
Ndugu
wanahabari,
Siku
ya Ukoma Duniani inatupa fursa ya kutathmini mwelekeo wa jitihada zetu nchini
na zile za kimataifa katika kupambana na ugonjwa huu. Kauli mbiu katika
maadhimisho ya mwaka huu ni “TUTOKOMEZE
UBAGUZI, UNYANYAPAA NA CHUKI DHIDI YA WAATHIRIKA WA UKOMA”. Ni kweli kuwa waathirika
wengi wa Ukoma wananyanyapaliwa na kubaguliwa katika maeneo mengi, takriban
asilimia 50 ya wagonjwa wa Ukoma hupatwa na sonona na huishi maisha ya huzuni
na wasi wasi mkubwa. Haya yote husababishwa na mtazamo hasi wa jamii dhidi ya
waathirika wa ugonjwa wa Ukoma. Mtazamo huu hasi ndio kikwazo kikubwa katika
vita ya kutokomeza Ukoma duniani na hapa nchini.
Serikali, wadau na wananchi wote wanahimizwa
kuungana na kuongeza nguvu katika kupinga matukio vyote vya ubaguzi na
unyanyapaa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hakuna sheria kandamizi kwa watu
walioathirika na ugonjwa wa Ukoma. Kwa kufanya kazi pamoja na kupinga kwa nguvu
zote vitendo hivi itatusaidia kupiga hatua mbele kuelekea kutokomeza Ukoma.
Ndugu
wanahabari,
Pamoja
na kwamba nchi yetu ilifikia viwango vya utokomezaji wa Ukoma kitaifa mnamo
mwaka 2006 kwa kiwango cha chini ya mgonjwa 1 kati ya watu 10,000, Ukoma bado unaendelea
kuwa tatizo la kiafya miongoni mwa jamii nchini kwetu. Kwa mujibu wa takwimu za
Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua kikuu na Ukoma (NTLP) za mwaka 2017, jumla
ya wagonjwa wapya 1,933 waligunduliwa na hivyo kufanya kiwango cha ugunduzi
kuwa watu 4 kwa kila watu 100,000. Takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuendelea
kuwa miongoni mwa nchi 22 zenye wagonjwa wengi wa Ukoma duniani nchi nyingien
ni pamoja na India, Indonesia, Brazil, Ethiopia, Msumbiji, Nigeria na DRC Kongo.
Hivi sasa bado kuna mikoa kumi ambayo inagundua wagonjwa wapya wa Ukoma wengi
zaidi kila mwaka na kuchangia karibia 80% ya wagonjwa wote. Mikoa hiyo ni
pamoja na: Lindi, Rukwa, Mtwara,
Morogoro, Pwani; Tanga, Geita, Dodoma, Tabora na Kigoma.
Aidha, bado zipo wilaya 20 ambazo kiwango cha
ukubwa wa tatizo la Ukoma lipo juu sana na bado hazijafikia lengo la
utokomezaji, nazo ni Liwale, Lindi vijijini, Nachingwea, Ruangwa, Nanyumbu,
Masasi mjini, Pangani, Mkinga, Korogwe, Mvomero, Kilombero, Morogoro vijijini,
Ulanga, Shinyanga manispaa, Mafia, Rufiji,
Kilwa, Chato, Nkasi, na Mpanda.
Ndugu wanahabari,
Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia
Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI inatekeleza shughuli
mbali mbali katika kuhakikisha Ukoma unatokomezwa kabisa. Shughuli hizo ni pamoja na :
·
Kuhakikisha dawa za kutibu Ukoma zinaendelea kupatikana wakati
wote na bila malipo yoyote,
·
Kuendesha
kampeni za uibuaji wa wagonjwa wapya
ngazi ya jamii kwa kuwashirikisha
watoa huduma ngazi ya jamii ( Leprosy Elimination Campaigns) hasa katika
wilaya zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa Ukoma,
· Kuendelea kutoa elimu
kwa jamii kuhusu dalili za Ukoma na upatikanaji wa huduma kwa kutumia vifaa vya
habari, Elimu na mawasiliano kama vile vipeperushi, mabango na mikanda ya video,
· Utekelezaji wa
shughuli za kuzuia ulemavu unaotokana na Ukoma ikiwemo kutathmini wagonjwa
wenye vidonda, kufanya upasuaji maalum, huduma za kitaalam za macho na utoaji
wa viungo bandia pamoja na viatu maalum.
Ndugu
wanahabari,
Pamoja na hatua zinazochukuliwa
na serikali na mafanikio zipo changamoto kubwa mbili ambazo ni jamii kuendelea
kushikilia imani potofu juu ya Ukoma kuwa ni ugonjwa wa kurithi au kulogwa; na
wagonjwa kuchelewa kujitokeza kupata matibabu hadi wanapopata ulemavu. Ukoma ni
ugonjwa wa kuambukizwa unaosababishwa na vimelea vinavyoshambulia mishipa ya
fahamu na huambukizwa kwa njia ya hewa pekee.
Nitoe
rai kwa jamii, wazazi na walezi kuwa sote tujenge tabia ya kuchunguza miili
yetu na ya watoto wetu. Endapo utaona mojawapo ya dalili za Ukoma ambazo ni
baka au mabaka mwilini yenye rangi ya shaba na hayana hisia, vijinudu kwenye
ngozi au mishipa ya fahamu kuvimba. Dalili nyingine ni ganzi kwenye mikono na
miguu. Unashauriwa kwenda kwenye kituo cha tiba kilicho karibu nawe kwa uchunguzi
bila kuchelewa. Hii itawawezesha wataalam wa afya kuchunguza na kubainisha kama
mgonjwa ana Ukoma ili apate tiba sahihi mapema na hivyo kuzuia maambukizi na
ulemavu wa kudumu unaoweza kuzuilika.
Ugonjwa
wa Ukoma unatibika. Mgonjwa aliyeanza tiba hawezi kuambukiza mtu mwingine na
hivyo hakuna sababu ya kumtenga na anaweza kuendelea na shughuli za kawaida za
maisha.
Tiba
ya Ukoma inapatikana nchini kote na hutolewa bila malipo kwa wagonjwa wote.
Nirudie
tena kuwa, pale tunapoona mabadiliko yoyote yanajitokeza kwemye miili yetu
twende mapema katika vituo vyetu vya huduma kuchunguzwa ili tupate matibabu
stahili.
Ndugu
wanahabari,
Aidha, napenda kuwashukuru watoa huduma
katika vituo vya huduma za afya kote nchini kwa juhudi wanazofanya kila siku
kuhakikisha ugonjwa huu si tatizo la kiafya tena nchini. Pia wanahabari kwa
kuendelea kuendelea kuelimisha jamii kuhusu magonjwa mbalimbali.
Pia nachukua nafasi hii kwa niaba ya serikali
ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli kuyashukuru mashirika mbali mbali ya ndani na nje yanayounga
mkono juhudi zetu za kutokomeza Ukoma nchini kama vile Norvatis Foundation ya
Uswisi, Germany Leprosy and Tuberculosis Relief Association (GLRA) ya
Ujerumani, Nippon Foundation chini ya
Sasakawa Memorial Health Initiative ya Japani na Shirika la Afya Duniani
(WHO) kwa michango yao ya hali na mali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa
Ukoma hapa nchini Tanzania.
“TUTOKOMEZE UBAGUZI, UNYANYAPAA NA CHUKI DHIDI YA
WAATHIRIKA WA UKOMA”.
Asanteni kwa kunisikiliza!



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...