Homa ya Maandalizi ya tamasha la 16 la Sauti za Busara imezidi kupanda, kwani wahudhuriaji kutoka ndani na wale wageni wa kimataifa wanajiandaa kwa ajili ya msimu mwingine wa muziki unaopigwa (live) mubashara kutoka katika kila kona ya bara la Afrika. 

Busara Promotions limethibitisha kuwa mpangilio wa tamasha hilo lililojizolea heshima kubwa miongoni mwa watu upo vizuri kwani lilianza rasmi siku ya Jumanne, Februari 7 na linaendelea. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Yusuf Mahmoud kauli mbiu ya tamasha la mwaka huu inalenga kupambana na rushwa kwa kuwa wanaamini wasanii wanaweza kutumia sauti zao kukabiliana na tatizo hilo wakati wanasheherekea utajiri na mkusanyiko wa tamaduni mbalimbali za muziki wa Afrika. 

“Katika kuunga mkono wasanii wanaotumia muziki kusimamia amani, umoja, haki za binadamu na uhuru wa kujieleza, ujumbe wenye nguvu ambao unaonekana katika tamasha la mwaka huu ni (“Potezea Rushwa, Sio Dili!),” alisema Mahmoud. 

Aliongeza kuwa, “Rushwa ni janga linalotafuna/ linalomomonyoa maadili ya jamii zetu barani Afrika na nje ya Afrika. Kibaya zaidi imefikia hatua kuwa hata baadhi ya watu wamekuwa wakichukulia ni jambo la kawaida. Hata hivyo, tamasha moja pekee haliwezi kubadili jamii yote kikamilifu, hivyo, tunashirikiana pamoja na washirika wa ndani na wa kimataifa kuendeleza majadiliano/mazungumzo, kubadili mitazamo na kuchochea hatua mbalimbali kwa ajili ya uongozi bora,” anasema Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara. 

Baadhi ya wasanii watakaounga mkono jitihada za kusambaza ujumbe wa kukabiliana na rushwa ni pamoja na Faith Mussa (Malawi), Fadhilee Itulya (Kenya), Fid Q (Tanzania), BCUC (Afrika Kusini) na wengineo watakaokuwa wakitumbuiza katika tamasha. “Hatua hizi ndogo ndogo zitasaidia kuweka muongozo mwishoni katika kuleta mabadiliko yale tunayoyakusudia kwa pamoja,” anasema Mahmoud. 

Meneja wa Tamasha la Sauti za Busara, Journey Ramadhan anasisitiza kuwa tamasha hili la Sauti za Busara linaendelea kuzitangaza Tanzania na Zanzibar ulimwenguni kote, kwa kuwa tamasha huvuta waandaaji wengi wa matamasha wa kimataifa, hivyo linatoa fursa kwa wasanii wa muziki wa Afrika Mashariki kusambaza muziki wao na kuifikia hadhira ya kimataifa. 
“Orodha yetu ambayo inaonekana kuwa ni ya kawaida sana lakini yenye utajiri mkubwa wa vipaji, inahusisha upekee wa sauti kutoka Zanzibar na Tanzania, pamoja na makundi yale yanayojiandaa kwa ajili ya kuudhihirishia ulimwengu mkusanyiko wa aina mbalimbali ya miziki ya wazawa hasa,” alisema Ramadhan. 

Tiketi za mwanzo bado zinaendelea kufanya vizuri katika mauzo na waandaaji wanaamini kuwa fedha hizo zitasaidia kugharamia kwa takriban asilimia 30 ya matumizi ya tamasha. Hata hivyo, licha ya kufanikiwa kwake katika miaka iliyopita, tamasha hilo kwa miaka ya hivi karibuni halikuweza kwenda vizuri kutokana na changamoto za ufadhili ambazo zinalifanya tamasha hilo liendelee kufanyika kwa bajeti hafifu/ndogo jambo linalosababisha hatua za uombaji msaada kwa wahisani. 

“Mvuto wa tamasha unaendelea kukua, licha ya vikwazo vya kifedha kuendelea kuliandama. Kumekuwa na msaada mdogo sana kutoka kwa Serikali kuhusiana na Sanaa hii. Sekta binafsi nazo bado hazifanyi masuala ya kuzisaidia jamii zinazowazunguka na ufanyaji harambee umekuwa mgumu kila mwaka. Wakati huo huo, ukilinganisha na matamasha mengine, tumekuwa tukiendelea kujiendesha kwa bajeti finyu huku tukiendelea kuweka kiingilio wanachomudu wazawa, mauzo ya tiketi yanagharamia asilimia 30 ya gharama zote,” anasisitiza 

Mkurugenzi wa Tamasha, Yusuf Mahmoud. Kipaumbele cha Tamasha la Sauti za Busara ni kuendelea kuwa tamasha ambalo Watanzania wanaweza kumudu kuhudhuria kwa gharama nafuu, hivyo kiingilio kwa mzawa ni Sh 10, 000

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...