Waajiri na Mamlaka za Ajira nchini watakaoshindwa kuwasilisha vielelezo vya rufaa zilizokatwa na watumishi wa umma kwenye Tume ya Utumishi wa Umma ndani ya siku 14 kama sheria inavyoelekeza watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuikwamisha Tume ya Utumishi wa umma kutekeleza jukumu lake la kushughulikia kwa wakati rufaa za watumishi.
Tahadhari hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma Makao Makuu ya Tume hiyo, akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya Tume na kujiridhisha namna Tume hiyo inavyotekeleza majukumu yake.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, kitendo cha waajiri kutowasilisha vielelezo vinavyohitajika na Tume ya Utumishi wa Umma kwa wakati ili kuiwezesha Tume kufanya maamuzi sahihi ya rufaa imekuwa ni kikwazo cha utekelezaji wa majukumu ya Tume, ambayo moja ya jukumu lake ni kusimamia, kufuatilia na kutathmini uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma nchini.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameisisitiza Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Umma kuhakikisha inatoa elimu kwa umma kuhusu utaratibu wa kufanyia kazi rufaa zinazowasilishwa ili waweze kujua ni muda gani unaotumika kushughulikia rufaa zao, na kuongeza kuwa elimu hiyo itapunguza malalamiko dhidi ya Tume kuwa haifanyii kazi rufaa zao kwa wakati.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameelekeza kuwa, kuanzia sasa ni marufuku kwa mwajiri yeyote kumhamisha mtumishi aliyebainika kuwa na kosa mahala pa kazi, kwasababu Tume ya Utumishi wa Umma itashidwa kushughulikia suala la mtumishi huyo na kuna uwezekano mkubwa akafanya tena makosa yale yale anakohamia.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Richard Odongo amesema kuwa, majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma yameainishwa katika Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 Kifungu 10 (1) ambapo imepewa mamlaka ya kutoa miongozo na kuhakikisha Utumishi wa Umma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.
Bw. Odongo ameendelea kufafanua kuwa,Tume ya Utumishi wa Umma ni mamlaka ya rufaa kwani inapokea na kushughulikia rufaa za watumishi wa umma, hivyo inafanya kazi kama mahakama ndani ya Utumishi wa Umma na ni chombo cha kutoa haki kwa watumishi wanaoonewa, na kuongeza kuwa, Tume inasimama kama mdhamini kuhakikisha haki inatendeka pande zote yaani kwa mwajiri na mtumishi.
Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu, Dkt. Steven Bwana, amemshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa maelekezo ya kuboresha utendaji kazi aliyoyatoa na kuahidi kusimamia utekelezaji wake.
Tume ya Utumishi wa Umma iliundwa kwa Mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 ili kuhakikisha kuwa, Utumishi wa Umma unakuwa mmoja na watumishi wote wanakuwa na taratibu za usimamizi, hadhi, haki na masilahi yanayofanana.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Tume ya
Utumishi wa Umma (hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi Makao Makuu
ya Tume hiyo Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhimiza
uwajibikaji.
Kaimu
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Richard Odongo akieleza
majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi
wa Tume chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kilichofanyika Makao Makuu
ya Tume hiyo yaliyopo Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma wakimsikiliza Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha
Naibu Waziri huyo na watumishi hao cha kuhimiza uwajibikaji
kilichofanyika Makao Makuu ya Tume hiyo yaliyopo jijini Dar es Salaam.
Kaimu
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Richard Odongo akifafanua jambo
kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kuhusu utekelezaji wa
majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma, wakati wa kikao kazi cha Naibu
Waziri huyo na watumishi wa Tume chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji
kilichofanyika Makao Makuu ya Tume hiyo yaliyopo Ubungo Plaza jijini
Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu, Dkt. Steven Bwana,
akifafanua majukumu ya bodi yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) wakati wa kikao kazi na Naibu Waziri huyo na watumishi wa
Tume ya Utumishi wa Umma chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji
kilichofanyika Makao Makuu ya Tume hiyo yaliyopo Ubungo Plaza jijini Dar
es Salaam.
Kaimu
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Richard Odongo akielezea
mchakato wa kushughulikia rufaa kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) aipotembelea moja ya ofisi zinazofanyia kazi rufaa
zinazowasiliswa Tume ya Utumishi wa Umma.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na
Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Umma, mara baada ya kumalizika kikao
kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa Tume hiyo cha kuhimiza
uwajibikaji kilichofanyika Makao Makuu ya Tume hiyo Ubungo Plaza jijini
Dar es Salaam.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...