Ujumbe wa wawekezaji wa makampuni makubwa 15 ya Saudi Arabia utafanya ziara nchini Tanzania tarehe 30 na 31 Januari 2019 kwa madhumuni ya kuangalia fursa ya kuwekeza kwenye viwanda.

Ziara hiyo inatokana na juhudi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Saudi Arabia na wadau wengine  wa kushawishi wafanyabiashara wakubwa kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.

Ujumbe huo wa watu 20, utakapokuwa nchini pamoja na mambo mengine, utashiriki kongamano la biashara litakalofanyika kwenye Hoteli ya New Africa jijini Dar Es Salaam tarehe 30 Januari 2019 kuanzia saa mbili asubuhi. Kongamano hilo litafuatiwa na mazungumzo ya ana kwa ana baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Saudi Arabia.

Kongamano hilo linaloratibiwa na Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) litatoa fursa kwa wafanyabiashara hao kusikiliza mada mbalimbali kuhusu fursa, vivutio, sheria na kanuni za uwekezaji nchini kutoka taasisi zinazoratibu masuala ya uwekezaji ikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Ujumbe huo pia unatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi mbalimbali; zikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TANTRADE), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Uwekezaji na Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).

Ziara ya ujumbe huo ni moja ya mikakati ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi na inalenga kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda ili kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
29 Januari 2019
  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...