Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
TAASISI ya Girl in Action Initiative imezindua kampeni ya siku 40 iliyopewa jina la
Msitiri Mtoto wa Kike ambapo kupitia kampeni hiyo wanatarajia kukusanya nguo za
ndani pamoja na sidiria ambazo zitagawiwa kwa watoto wa kike na hasa wanafunzi.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ya Msitiri Mtoto wa Kike
Mwanzilishi wa taasisi hiyo Miriam Lukindo Mauki amesema wameizundua kampeni
hiyo leo na itafika tamati Machi 13 mwaka huu huku akifafanua asilimia kubwa ya
wanafunzi wanatoka kwenye familia zenye kipato cha chini ambapo inafika wakati
wanashindwa hata kupata fedha ya kununulia nguo za ndani(Chupi na Sidiria).
"Msitiri wa mtoto wa kike ni kampeni iliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya kumsaidia
mtoto wa kike ambaye yuko shuleni ili aweze kufikia ndoto yake ya kupata elimu na
kampeni hi inazinduliwa leo rasmi Februari 1 hadi Machi 13,2019,"amesema Miriam
Mauki kuwa kampeni hiyo imekuja baada ya kuona watoto wengi wa kike huwa
wanapata changamoto za kujisitiri katika maungo yao ya siri na hiyo kusababisha
wengi wao kukosa umakini na kujiamini wawapo madarasani.
Amefafanua Girl in Action Initiative imeona ni vema kuwasaidia hao watoto wa kike
kwa kidogo walichonacho ili kuhakikisha wanasoma kwa furaha na wanajisitiri
vyema na kuongeza ukimuinua mtoto wa kike umeinua jamii nzima na njia pekee ya
kumuinua mtoto wa kike ni kumpatia elimu.
"Ni ukweli usiopingika Serikali ya Awamu ya Tano inafanya jitihada kubwa
kuhakikisha vijana hasa wanawake wanapata elimu bora, na imesaidia kuingiza
taulo za kike bila kulipiwa kodi ili kumsaidia mtoto wa kike ajisitiri na hatimaye
asome kwa kufaraha na kuzifikia ndoto zake .
"Pamoja na hayo kuna changamoto ndogondogo ambazo zinaweza kuwa ni kikwazo
kwa mtoto wa kike kuzifikia ndoto zake kielimu.Kampeni hii itahusisha kukusanya
fedha pamoja na nguo za ndani kutoka kwa wasamaria wema, taasisi na asasi
mbalimbali ili kuhakikisha kila mtoto mwenye hitaji anafikiwa,"amesema .
Ameongeza kuwa kumjenga mtoto wa kike uwezo wa kujiamini, kumpatia mtoto wa
kike elimu ya kujisitiri na baadhi ya mahitaji katika muhimu ya kujisitiri na
kumsaidia kuwa huru na furaha ili aweze kufocus katika masomo yake."Kupitia
kampeni hii huku tukishirikiana na washika dau wetu na wapenda maendeleo ya
mtoto wa kike ili kuwafikia watoto wengi wa kike kadri inavyowezekana."
Miriam Mauki amesema ili kuifanikisha wanaomba kwa yeyote anayewiwa kuwa
sehemu ya kampeni hiyo anaweza kutoa mchango wake ambao ni kuanzisha
Sh.1000 kwa kutumia namba ya simu ya tigopesa 0677069428 ambayo imesajiliwa
kwa jina la Christom Solution na ni imani yake kama jamii itashirikiana kwa pamoja
wanaweza kufikia kampeni hiyo kwa kuwafikia hao watoto wa kike wengi zaidi.
Pia amefafanua kabla ya kuzinduliwa kwa kampeni hiyo walifanya utafiti na kubaini
kuna idadi kubwa ya watoto wa kike walioko shuleni hawana uwezo wa kununua
nguo za ndani na kwamba wakiwa Karatu walibaini kati ya watoto 400 ni wawili tu
ndio waliokuwa wamevaa sidiria na watoto hao ndio hata darasani wanaouwezo
mkubwa kuliko wengine kimasomo."Kampeni hii ya siku 40 lengo letu ni kuwafikia
watoto 1000, hivyo tunaomba jamii kushirikiana nasi kufanikisha kampeni hii."
Kwa upande wake Mmoja wa wahamasishaji wa kampeni hiyo Sadaka Saidambaye
pia ni Mkurugenzi Mtendaji Family Dynamics ametumia nafasi hiyo kuiomba jamii ya
Watanzania kujitokeza kuchangia ili kufanikisha kupata nguo hizo na hatimaye
kutatua changamoto iliyopo kwa wanafunzi hao.
Ametoa ombi kwa wanaohitaji kuchangia ni vema kabla ya kununua sidiria
wakawasiliana Girl in Action Initiative ili kupata saizi ya sidiria lakini kwenye nguo ya
ndani hizo hazina shida sana huku naye akisisitiza namba ambayo inapaswa
kutumika kutuma fedha ni hiyo ya tigopesa lakini wanaendelea kufanya mazungumzo
na kampuni nyingine za simu ili kuwasaidia namba ambazo zitatumika kutumia
fedha hizo.
"Mtoto wa kike anapojisitiri maungo yake ya siri kuna faida nyingi, kwanza
anajiamini sana na anakuwa hana wasiwasi lakini pia mtoto wa kike hasa
aliyepevuka anapojisitiri mwili anajiepusha na mafisi ambao wao wakiona tu mwili
wa binti wanaingiwa na tamaa na wakati mwingine kufanya ubakaji,"amesema.
Wakati huo huo Mhamasishaji mwingine wa kampeni hiyo ambaye ni MC Mkongwe
Sisila Ngalemwa amewataka wazazi wa kiume kuwasiliza watoto wao wa kike ikiwamo
kuwasaidia kifedha kununua mahitaji yao muhimu yanayohusu kujisitiri.
Amesema kuwa wapo baadhi ya watoto wa kike wamekuwa na ukaribu mkubwa kuliko
mama zao, hivyo ukaribu huo wazazi wa kiume wautumie kuzungumza na watoto zao
wa kike huku akishauri ni vema kukawa na bajeti maalumu ya mtoto wa kike ya kila
mwezi.
"Miaka ya nyuma ilikuwa ni ngumu mtoto wa kike kukaa na baba yake lakini siku hizi
ni jambo la kawaida mtoto wa kike kuwa karibu na baba yake , sababu ziko nyingi na
mojawapo ni kwamba anapokuwa na mama kuna baadhi ya mambo wanatofautiana. Kwa mfano mtoto anaweza kuambiwa osha viombo na anapoonesha kutokuwa tayari
lazima mama atachukia lakini kwa baba anaona ndio kimbilio lake. Hivyo ni vema
wazazi wa kiume watumia nafasi hiyo kuwasaidia watoto wao,"amesema.
Mhamasishaji wa Kampeni ya Msitiri Mtoto wa Kike MC Reeves Sisila Ngalemwa (wa kwa za kulia)akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo yenye lengo la kukusanya nguo za ndani ili kuwapelekea watoto wake na hasa wanafunzi wenye mahitaji.
Mhamasishaji wa Kampeni ya Msitiri Mtoto wa kike Sadaka Said(watatu kulia) akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo iliyozinduliwa leo jijini Dar es Salaam.
Mwanzilishi wa Girl in Action Initiative(wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa kampeni ya Msitiri Mtoto wa Kike iliyozinduliwa leo jijini Dar es Salaam.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...