Na Estom Sanga- DSM
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Dr. Moses Kusiluka amesema Serikali inatambua Mchango muhimu unaotolewa na nchi wahisani na Wadau wa Maendeleo katika kufanikisha jitihada za Serikali za kukabiliana na umasikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF.
Dr. Kusiluka amesema jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwaondolea wananchi adha ya umaskini zimeendelea kufanikiwa na kupongeza ushirikiano uliopo baina ya Serikali kupitia TASAF na Wadau wa Maendeleo ambao amesema unapaswa kuendelezwa ili kuwanufaisha Wananchi.
Katibu Mkuu huyo wa Ofisi ya Rais ameyasema hayo alipokutana na Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF na Wadau mbalimbali wa Maendeleo katika ofisi ndogo za Mfuko huo jijini Dar es Salaam katika kikao ambacho hufanyika kila mwezi kujadili utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo.
Dr. Kusiluka amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuendelea kusimamia na kutekeleza kwa karibu Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF ili jitihada hizo na nyingine ambazo zinafanywa na Serikali zinazolenga katika kupunguza umaskini uliokithiri miongoni mwa wananchi ziweze kufanikiwa na kuwa endelevu.
Amewahakikishia Wadau hao wa Maendeleo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatambua Mchango wao katika kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF na kuwa itaendelea kushirikiana nao katika kufanikisha malengo ya Mpango huo ambao kwa kiwango kikubwa unaonyesha mafanikio.
Akizungumza katika kikao kazi hicho Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF bwana Ladislaus Mwamanga amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini yametokana na ushirikianao wa Serikali na Wadau hao wa Maendeleo ambao Wamewezesha kuzihudumia takribani Kaya Milioni Moja na Laki moja ambayo ni asilimia 70 ya vijiji na shehia nchini kote kwa ufanisi .
Kwa upande wa Wadau hao wa Maendeleo ,Kiongozi wa Shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia hapa nchini Bw.Mohamed Muderis amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa Wadau wa Maendeleo kuendelea kuchangia utekelezaji wa Shughuli za TASAF kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kuipongeza Serikali kwa usimamizi wa karibu ambao umesaidia kupatikana kwa mafanikio hayo.
Hata hivyo Bw. Muderis ameishauri serikali kupitia TASAF kuweka mkakati thabiti utakaowezesha sehemu ya pili ya utekelezaji wa Awamu ya tatu unaotarajiwa kuanza hivi karibuni kuwa na mtiririko mzuri wa fedha za kugharamia shughuli za Mpango kutokana na kuwa utatekelezwa katika maeneo makubwa zaidi ya awamu inayomalizika na hivyo kuhudumia Walengwa wengi zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga(kushoto)
akimkaribisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Dr. Moses Kusiluka (kulia) katika ofisi
ndogo ya mfuko huo jijini Dar es Salaam ambako amekutana na Wadau wa Maendeleo
na Uongozi wa TASAF.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Dr. Moses Kusiluka (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bwana Ladislaus Mwamanga (kushoto) wakiwa katika kikao kazi cha Wadau wa Maendeleo na Menejimenti ya TASAF katika ofisi ndogo ya Mfuko huo jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Wadau wa Maendeleo na Menejimenti ya TASAF wakiwa katika kikao kazi ambacho pia kimehudhuriwa na Katika Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Dr. Moses Kusiluka kujadili utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...